Mwenyekiti wa tume ya AU, ametoa wito kwa mataifa ya Afrika kuchukua hatua madhubuti za kupambana na tisho la usalama linalotokana na kundi la Boko Haram.
Nkosazana Dlamini-Zuma ameambia kikao cha AU kinachoendelea nchini Ethiopia, kwamba unyama unatotendwa na kundi hilo sio tisho tu kwa Nigeria bali kwa bara zima.
Mkutano wa wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika umeanza leo nchini Ethiopia ambapo viongozi wa Afrika wanatarajiwa kujadili masuala muhimu yanayolikumba bara la Afrika kwa sasa.
Baadhi ya maswala yatakayopewa kipaombele kwenye mkutano huo ni tisho la usalama linalotokana na Boko Haram nchini Nigeria, pamoja na juhudi za kupambana dhidi ya ugonjwa hatari wa Ebola.
Licha ya kauli mbiu ya mkutano huo wa siku mbili kuwa swala la kuwawezesha wanawake, viongozi kutoka nchi 54 wanachama wa Muungano huo watalazimika kuangazia swala la migogoro ambalo limekuwa changamoto kubwa kwa bara la Afrika.
Mnamo siku ya Alhamisi, baraza la usalama na amani la AU, lilitoa wito wa haja ya kuwepo kikosi cha wanjeshi 7,500 kupelekwa katika maeneo yanayokumbwa na migogoro Afrika.
Wakati huo huo Kenya inatarajia kutuma ujumbe mzito kwenye mkutano huo kama mwanzo wa hatua yake ya kukata uhusiano na Mahakama ya jinai ICC.
Katika kikao kilichopita cha Umoja wa Afrika kilichokaa mjini Malabo Equatorial Guinea wajumbe walisaini mkataba wa uundwaji wa mahakama ya Afrika itakayoshughulikia kesi za Afrika badala ya kuzipeleka kwenye mahakama ya ICC, baadhi yao wakidai kuwa kesi za mahakama hiyo zinawalenga waafrika pekee.
No comments:
Post a Comment