‘Umoja’ wa ukoloni haudumu - LEKULE

Breaking

20 Dec 2014

‘Umoja’ wa ukoloni haudumu

NAPENDA kuhitimisha ngwe hii ya makala hizi (ambazo zimekuwa na mada kuu ya serikali za mitaa) kwa kuelezea baadhi ya hoja zilizoibuka kutokana ama na hoja niliyokuwa nikiijenga wakati wote huu ama kutokana na maswali niliyoulizwa na baadhi ya wasomaji waliotaka kujua nafikiri nini kuhusu vipengele kadhaa katika hoja hiyo.

Kwanza sina budi kusema kwamba ninachokisema si kipya, kimewahi kusemwa mara nyingi, na kimesemwa na watu wenye umahiri mkubwa zaidi wa kueleleza masuala kuliko nilio nao. Wanazuoni na wanataaluma mbali mbali za kijamii wameliandikia suala hili la madaraka ya wananchi katika maandiko mengi yenye weledi mkubwa.

Katika nchi jirani ya Kenya hoja hii imekuwa miongoni mwa hoja kuu za mjadala wa kimsingi kuhusu jinsi Wakenya wanavyotaka kujitawala. Katika nchi hiyo hili ni suala lililodumu kwa muda mrefu sana, tangu miaka ya 1960, mara tu baada ya Uhuru wa Kenya, wakati ule likijulikana kama u-majimbo (majimboism).

Hivi karibuni, Wakenya, ambao mara nyingi wanatutangulia katika kutohoa maneno ya lugha ambayo tunadai ni yetu kuliko ilivyo yao, wametambua neno jingine, ‘ugatuzi,’ kuelezea dhana hiyo hiyo. (Tukumbuke pia kwamba walituletea neno UKIMWI).

Aidha, katika nchi nyingi na kupitia karne kadhaa katika historia ya binadamu, hamu ya watu wa eneo mahsusi kutaka kujiamulia mambo yao wenyewe, hata kama wanakubaliana kwamba baadhi ya mambo yanaweza yakachangiwa kwa pamoja na watu wengine, imekuwa na msukumo mkubwa ambao kila usipotambulika na kutafutiwa ufumbuzi, umezua zahma ambazo zingezuilika endapo wahusika wangetambua tatizo liko wapi.

Tatizo liko wapi? Swali hili nimelijibu mara kadhaa katika makala hizi, lakini si vibaya kulieleza kwa maneno mengine. Tatizo liko katika ugawanaji wa madaraka kati ya utawala wa juu(au kati) na utawala wa chini (au pembezoni), kati ya serikali kuu iliyoko makao makuu ya nchi na serikali ndogo ndogo za wananchi walioko katika maeneo yao.

Tatizo liko ndani ya historia, ambayo kwa hakika inatuambia kwamba ingawaje tumelundikwa pamoja kwa nguvu za wakoloni na kwa maslahi na mahitaji yao, bado tumebeba mizigo ya utambulisho wetu, bado tunazo tofauti zetu ambazo utambuzi wake ni nyenzo muhimu katika kutuleta karibu, na kujifanya hazipo ni kujidanganya.

Tatizo liko ndani ya dhana iliyojengeka kwa muda mrefu (bila kusemwa bayana) kwamba yapo masuala nyeti ambayo ni mwiko kuyajadili, na hivyo ni bora kuyaacha “kama yalivyo”. Hii imejengeka katika woga wa kujadili mambo ambayo hata kama ni dhahiri yanahitaji kujadiliwa, ni wachache wanathubutu kuchokoza mjadala juu yake. Ni ile dhana ya “ka kitandugaho” ninayoizungumzia mara kwa mara.

Pasi na shaka inazuka hoja ya ‘ukabila,’ baadhi ya watu wakitoa hoja kwamba kuimarisha serikali za mitaa kwa kuwekeza katika ‘ugatuzi’ ulio makini zaidi kutawafanya wananchi wajenge hisia za kikabila zaidi kuliko za kitaifa na hivyo kudhoofisha umoja wa kitaifa. Hoja hii inavutia kwa kiasi fulani na haina budi kupewa uzito inaostahili:

Tukiangalia nchi zetu nyingi barani Afrika tunashuhudia migawanyiko mingi na mikubwa iliyosababisha mitafaruku mikubwa miongoni mwa watu wake. Mara nyingi mitafaruku hii hubebeshwa maelezo ya juu juu kutokana na watu wanaoiangalia na kuitafakari, mara nyingi wakiwa hawana muda wala sababu za kuangalia masuala yaliyojificha ambayo labda yana umuhimu mkubwa kuliko vielelezo vinavyojitokeza kwa mpita- njia.

Nitapata wasaa wa kulirejea suala hili katika makala zijazo, lakini hapa inatosha kusema kwamba kuwanyima wananchi madaraka ya kuamua mambo yao si njia ya kuua hisia za kikabila, bali inaweza kuwa ndiyo njia mwafaka ya kuzichochea. Imetokea mara nyingi kwamba mambo yanayofanywa kwa nia njema lakini iliyopotoka ili kuzuia jambo fulani yanaweza hayo hayo yakawa ndicho chanzo cha jambo lililokusudiwa kuzuiwa.

Utambulisho wa ‘kikabila’ ndio utambulisho wa ngazi ya juu tuliokuwa tumefikia katika ‘makabila’ yetu yaliyo mengi. Katika maeneo machache barani Afrika tulikwisha kufikia ngazi ya juu zaidi kuliko kabila, tukawa na ‘falme’ zilizojumusiha ‘makabila’ kadhaa, falme hizi zikiwa ni matunda ya mapambano ya kivita baina ya makabila ya eneo moja. Haina tofauti sana na jinsi mataifa ya Ulaya yalivyojijenga na yalivyojenga falme zake.

Kwa maana hii Uhehe, Unyanyembe na sehemu chache nyingine ndani ya Tanganyika, na kwingineko Buganda, Manikongo, Zulu, Songai, Ashanti, na nyingine chache barani Afrika zilikuwa ni himaya zilizokwisha kukiuka mizingo finyu ya kabila na kuyaweka makabila kadhaa chini ya utawala wa ufalme mmoja. Haya ndiyo yalikuwa mataifa ya kweli ya Kiafrika, mara nyingi, kama huko Ulaya, yakiletwa pamoja kwa nguvu za kivita za mtawala mmoja mwenye visheni ya kuwaunganisha.

Hata hivyo himaya kama hizi zilikuwa chache mno, na ujio wa wakoloni haukuziruhusu zishamiri kwani mara moja zilipondwa, zikavunjwavunjwa na zikawekwa chini ya ‘uangalizi’ wa wakoloni na zikafanywa zitumikie maslahi ya wakoloni kupitia mifumo na mitandao ile ile zilizokuwa zimejenga.

Zilikuwapo pia tawala nyingine, dhaifu kuliko himaya hizo nilizozieleza hapo juu, na hizi ndizo zilikuwa nyingi zaidi, kwani si maeneo mengi ya Bara la Afrika yaliwahi kuwekwa chini ya himaya kubwa kama za Chaka, Mkwawa, Kabaka, Ashantihene, au Almamy. Nyingi miongoni mwa tawala zetu zilikuwa ni za makabila madogo madogo ambayo hata yalipopigana vita hakuna moja lililoweza kuwaweka wenziwe chini ya himaya yake kwa muda mrefu.

Ujio wa wakoloni ndio ulioyaleta makabila yote haya, (yaliyokuwa chini ya himaya kubwa za akina Mkwawa na yale yaliyokuwa katika vikabila vidogo vidogo), chini ya himaya moja kubwa katika maeneo waliyojigawia Wazungu mjini Berlin mnamo 1884-85. Miongoni wa hizi himaya na haya makabila hakuna aliyeulizwa kama alitaka ‘kuunganishwa’ na ye yote mwingine, alimradi mistari ilikwisha kuchorwa huko Berlin na mabwana zetu wamefika na wamekusudia kuunganisha mali yao.

Kwa hakika huu haukuwa msingi imara wa umoja wa nchi zetu kwa sababu hali yetu mpya haikutokana na mchakato wo wote tuliouelewa, si kwa vita, si kwa maridhiano miongoni mwetu. ‘Umoja’ tuliobambikizwa na wakoloni kwa kuwekwa ndani ya pakacha moja kama koloni (Tanganyika, Kongo, Sudan, Senegal, nk.) ni umoja bandia uliofinyangwa kwa maslahi ya wageni.

Ili ‘umoja’ huo uwe na uhalisia wo wote hauna budi kutiwa ‘udhu’ wa utashi wa wananchi wa nchi husika. ‘Udhu’ huu hauwezi kupatikana kwa kung’anga’nia mifumo chakavu ambayo kwa nusu karne imeshindwa kuonyesha mwelekeo wa maendeleo, wala hatuwezi kuzuia ukabila kwa “kuzuia ukabila,” kama vile ambavyo hatuwezi kudumisha amani kwa “kufanya kazi ya “kudumisha amani” . Katika mahusiano ya kijumuiya yapo mambo mengi ambayo hayapatikani kwa kuyafanya, bali hupatikana kama matokeo ya mambo mengine ya msingi yaliyofanyika. Mojawapo ni hili.

Ili kujenga umoja wa kweli ni lazima tuweke misingi ya kuheshimiana na kujaliana. Misingi hii haiwezi kudumu kama hatukuweka utaratibu unaowawezesha wananchi kujiamulia jinsi ya kuendesha maisha yao na kujiletea maendeleo. Hili haliwezekani iwapo hatuimarishi serikali za mitaa kama chombo cha wananchi.

No comments: