Zenawi alivyowashushua manabii wa injili ya ubinafsishaji na utandawazi. - LEKULE

Breaking

6 Nov 2014

Zenawi alivyowashushua manabii wa injili ya ubinafsishaji na utandawazi.


NINGEPENDA sana watawala wetu wafike Addis Ababa, Ethiopia wakiwa na macho yaliyofunguka tayari kwa kuona na kujifunza.

Kwa siku takriban sita nimekuwa, kwa mara nyingine, nikivinjari jiji hili na kujionea maajabu wanayoyafanya wananchi wa Ethiopia na Serikali yao, hususan katika ujenzi wa barabara, nyumba za kuishi na majengo ya ofisi.

Ni maajabu matupu kwa mtu aliyeujua mji huu kihistoria. Mara ya kwanza kwangu kuliona Jiji la Addis ilikuwa ni Januari, mwaka 1970. Nilikuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), mwaka wa kwanza, na nikapata fursa ya kuwakilisha Jumuiya ya Wanafunzi UDSM, katika mkutano wa “UN Decade of Africa’s Development”.

Mkutano uliohusisha jumuiya za kiraia na vyama visivyokuwa vya kiserikali. Nilipata nafasi ya kuutembelea mji huu na kujionea jinsi ulivyokuwa mchafu na usiopendeza sana. Tangu wakati huo nimekuwa nikirejea Addis mara kwa mara katika kipindi chote cha miaka 40 ‘ushei’.

Wakati wote mji ulikuwa ukionyesha dalili za maendeleo, lakini hayakuwa ya kasi kubwa. Itakumbukwa kwamba mji huu uliasisiwa na Mfalme Menelik wa Pili, mnamo mwaka 1889, na kwa kuwa Ethiopia haijawahi kutawaliwa kikoloni, mji huu haujawahi kuwa na maeneo yaliyotenganishwa kufuata rangi ya wakazi wake, kama vile miji yetu ilivyo na ‘Uzunguni,’ ‘Uhindini’ na ‘Uswahilini.’

Hii imekuwa na maana kwamba hakuna Oyster Bay, Upanga na Ilala, kwani sehemu zote za mji zina kila kitu. Si ajabu kuwa ghorofa ya kumi ya hoteli kama Sheraton na kuangalia chini ukaona ni soko wanakochinjwa kondoo au ni vibanda vya walalahoi wanaokwenda haja katika choo cha shimo kilichositiriwa kwa pazia la gunia.

Lakini katika kipindi kisichozidi miaka saba Addis imeonyesha kasi kubwa ya maendeleo katika ujenzi na upanuzi na uboreshaji wa miundombinu kiasi kwamba inashangaza.

Kila kona ya jiji, barabara zinapanuliwa, madaraja yanajengwa, njia za kupita juu (flyovers) zinasimikwa na majengo yanainuka. Kwa ujumla, mji huu umekuwa ni saiti ya ujenzi. Wageni wakazi niliozungumza nao hapa wanasema kwamba hali iko vivyo hivyo maeneo ya shamba, kwamba barabara zinajengwa na kupanuliwa na wananchi wanajengewa nyumba za kuishi kwa bei nafuu.

Meles Zenawi, Waziri Mkuu wa Ethiopia, amesimamia kazi zote hizi akifuata falsafa yake inayosisitiza umuhimu wa Serikali kushiriki moja kwa moja katika shughuli za kiuchumi na si kuiachia sekta binafsi kama wanavyohubiri manabii wa injili ya ubinafsishaji na utandawazi.

Katika mkutano niliohudhuria hivi karibuni, Meles amesisitiza falsafa yake hiyo. Akifungua mkutano wa tano wa pamoja kati ya Umoja wa Afrika (AU) na Tume ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi wa Afrika (UNECA) maalumu kwa mawaziri wa fedha na uchumi Machi 26, 2012, Meles amedhihirisha kuudhiwa kwake na sera za kiliberali zinazozidumaza nchi za Afrika na kuwanyanyasa watu wake.

Mada ya mkutano huo ni,  “Kufungulia uwezo wa Afrika na kufanya Nguzo ya Ukuaji wa Uchumi wa Dunia.”  Meles alisema: “ Lazima tuyakomboe mawazo yetu kutoka kwenye pingu za uliberali mamboleo ambazo zimefukarisha fikra zetu na kuzuia maendeleo yetu. Itikikadi hii muflisi imedhoofisha mamlaka ya serikali za Afrika kufikia kiwango cha zenyewe kuwa kama kolokoloni tu katika nchi zao.

Wote tunakubaliana kwamba tunahitaji kuwa na mamlaka ambazo zinaingilia kati  kwa uthabiti na tija, pale ambako masoko yanayumba na kutishia maendeeleo. Hiyo inawezekana tu kama tutaachana na hadithi zinazozitaka mamlaka kuendelea kuwa kama walinzi wa usiku.”

Meles aliongeza kusema kwamba kuna umuhimu wa kuwekeza kikamilifu katika ujenzi wa miundombinu kwa kutumia rasilimali za dola na kuachana na dhana ya kiliberali kwamba jukumu hili zito ni la sekta binafsi: “Tunahitaji kuwekeza sana katika miundombinu, na mara nyingi kupitia katika taasisi za umma.  Hivyo ndivyo miundombinu ya mataifa mengine yaliyoendelea ilivyojengwa. Itikadi hiyo inasisitiza kwamba miundombinu ijengwe na taasisi binafsi na maamlaka ziweke mazingira ya kuziwezesha taasisi hizi za binafsi kuwekeza bila kuingia hasara. Hiyo ndiyo sababu ya kwa nini kuna uwekezaji duni katika mindombinu katika bara lote la Afrika katika miaka 30 iliyopita.  Ni lazima tuvunje pingu hizi za kiitikadi na tushiriki katika uwekezaji mkubwa katika miundombinu huku wakati huohuo tukihimiza sekta binafsi kuwekeza katika maeneo inayoweza kuwekeza.”

Vivyo hivyo katika sekta ya elimu, Meles amelaani sera za kiliberali kuhusu dhima ya dola katika elimu, ambayo inataka serikali isimamie elimu ya msingi tu, na kwa kiasi kidogo elimu ya sekondari, lakini elimu ya juu iachwe kama jukumu la sekta binafsi na igharamiwe na familia moja moja.

Anatoa mwito wa kuikataa dhana hii na kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika elimu ya juu sambamba na uwekezaji katika elimu ya msingi: “Lazima tuondokane na dhana hii ya uliberali mamboleo kwa kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika elimu ya juu, vyuo vya ufundi, vyuo vya ufundi stadi na katika elimu ya sekondari na msingi na kuhamasisha sekta binafsi kuziba mianya ya uwekezaji huo  itakayojitokeza.”

Alisema kwamba sera hizo hizo zilizoiumiza Afrika na kuziumiza sehemu nyingine duniani ndizo hizo hizo zilizorudi kuziumiza nchi za magharibi ambao uchumi wake uligeuzwa uchumi wa ‘casino’ na kusababisha mtikisiko mkubwa wa kiuchumi katika nchi za magharibi na duniani kote: “Mfumo wa uliberali mamboleo ulioharibu uchumi wa nchi zetu sasa umegeukia katika baadhi ya mataifa yaliyokwishakuendelea, ukabadili taasisi za fedha za nchi hizo kuwa kama  majumba ya kuchezea kamari na hali hiyo ndiyo iloyochangia katika matatizo ya sasa ya kiuchumi katika nchi hizo.

Kwa upande mwingine, Meles anaona fursa za wazi zikijitokeza kuinufaisha Afrika iwapo nchi za Kiafrika zitazitambua na kuzichangamkia. Fursa hizi zinatokana na hali inayojidhidhirisha ya uchovu wa nchi zilizoendelea ambazo hazina nafasi ya kuwekeza tena, na ambazo haziwezi kujinasua pasipo kusaidiwa na nguvu mpya itakayotokana na fursa mpya za uwekezaji zitakazopatikana barani Afrika.

“Afrika, yenye zaidi ya watu bilioni moja na yenye uhitaji mkubwa wa uwekezaji tangu kwenye miundombinu hadi kwenye huduma za jamii ndiyo pekee inayoweza kuziba pengo katika mahitaji makubwa ya dunia.  Hazina kubwa ya akiba ya dunia ambayo sasa inaonekana kuwa ni tatizo, sasa inaweza kuwa ni suluhisho la matatizo kama itawekezwa katika bara la Afrika.”

Kwa kuzitumia vyema fursa zinazojitokeza, Meles anaamini kwamba laana za miaka ya 1980 zinaweza kugeuka kuwa baraka kwa Waafrika kutumia vyema fursa hizo, rasilimali maridhawa na ukubwa wa nguvukazi ya Waafrika, kujenga misingi imara ya uchumi wa viwanda.

No comments: