Mtoto wa Ulaya alivyofanikisha kuchangisha mamilioni kwa watoto wa Tanzania - LEKULE

Breaking

22 Nov 2014

Mtoto wa Ulaya alivyofanikisha kuchangisha mamilioni kwa watoto wa Tanzania

Huyu pichani juu  ndiye LUKEMAN CATER.


APRILI mwaka huu niliandika hapa habari za mtoto Lukeman Carter mwenye umri wa miaka 11 wa Norwich nchini Uingereza.

Kwamba mtoto huyu  aliijiwa na wazo la kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia watoto wa kijijini Mahango, Madibira mkoani Mbeya.

Azma ya mtoto huyu ilikuwa ni  kusaidia ujenzi wa chumba cha darasa ambalo pia lingetumika kama maktaba ya vitabu vya watoto wa chekechea, darasa la kwanza, la pili na la tatu.

Wazo la mtoto Lukeman Carter lilimjia baada ya kuguswa na picha kupitia mtandao wa Mjengwa Ni picha zilizoonyesha  mazingira magumu ambamo watoto wanapata elimu hapa Tanzania. Na mama  mzazi wa Lukeman, Bi Karrima Carter amezaliwa na kukulia Tanzania.  
    Lukeman alijiwekea lengo la kukusanya shilingi za Kitanzania milioni moja.  Mwitikio ukawa mkubwa kuliko alivyotarajia Lukeman na wengine. Sasa fedha alizochangisha zimefikia  shilingi milioni nne na maboksi zaidi ya 35 ya vifaa vya shule ikiwamo vifaa vya michezo. Michango zaidi imeahidiwa kwa mtoto huyo hata mwakani.

Michango hiyo inapitia kwenye taasisi ya kihisani iliyoundwa kwenye mji wa Norrwich kwa ajili ya kuchangisha misaada ya kihisani kwa watu wa Madibira na maeneo ya jirani kwenye bonde la Usangu. Na hapa nyumbani kuna wengi wengine waliomuunga mkono Lukeman Carter. Kupitia Mjengwa blog zimechangwa takribani shilingi milioni nne kupitia huduma za kutuma fedha kwa njia ya simu.

Kusafirisha maboksi hayo ya misaada iliyokusanywa na Lukeman na Bi Karrima Carter kufika Tanzania ingekuwa ni gharama kubwa sana.

Lakini, Mtanzania, mzalendo Chris Lukosi na wenzake wa kampuni ya Kitanzania ya usafirishaji yenye makao yake nchini Uingereza ya Serengeti Freighters and Forwarders ama maarufu kama ' Wazee Wa Kazi',  wameipokea mizigo hiyo kutoka kwa Bi. Karrima Carter na wamejitolea kusafirisha bure mizigo hiyo ya misaada kuja nchini Tanzania.

Hakika, huo ni uzalendo uliokidhi viwango. Bila shaka, msaada huu utasaidia kubadilisha maisha ya wengi kijijini Mahango na vijiji vya jirani kule Madibira, Mbarali Mbeya.

Watanzania tuna ya kujifunza kutoka kwa mtoto huyu, Lukeman Carter, maana, fedheha iliyopo Tanzania ni kuwa wafadhili kutoka Ulaya na Marekani wakishaona hali ya hizi shule zetu, wanajituma kuchangia na kuboresha hali hizo. Je, sisi wenyewe tunachukua hatua gani?

Niliandika huko nyuma, kuwa ni wakati sasa wa kujiuliza ni namna gani tunaweza kujenga mfumo utakaohakikisha kunakuwapo na udhibiti wa mapato na matumizi ya fedha za Serikali ambazo kimsingi ni fedha za wananchi.

Udhibiti hapa una maana moja kubwa. Kuwa, kama nchi,  tutaweza kujijengea uwezo wa kiuchumi kwa kutegemea vyanzo vyetu vya mapato. Ni uwezo kama huo utakaosaidia kuboresha sekta muhimu kama afya, elimu na miundombinu.

Lakini, kama wananchi, jukumu la kujiletea maendeleo haliwezi kubaki kwa Serikali na wahisani tu. Tuna wajibu wa kuchangia maendeleo yetu.

Bahati mbaya, Watanzania tumekuwa wagumu sana wa kuchangia shughuli zetu za maendeleo. Tumekuwa wagumu hata wa kufanya shughuli za kujitolea. Ikumbukwe, kuna watu wa kutoka Ulaya na Marekani ambao wako nchini mwetu na wengine wakiishi vijijini wakifanya kazi za kujitolea kwa maendeleo ya watu wetu.

Huko katika nchi zao  wanachangisha fedha. Si kwamba wao wana fedha nyingi sana na kuwa hawana matatizo. La hasha! Leo hali ngumu ya kiuchumi hapa duniani imezikumbuka hata nchi za Ulaya na Marekani, hivyo basi, raia wake pia. Hata hivyo, pamoja na matatizo ya uchumi yalivyo, wanahangaika ili walete misaada kwenye jamii yetu.

Kwa nini basi tumekuwa wagumu wa kuchangia shughuli za maendeleo yetu wenyewe? Badala yake, tumekuwa wepesi wa kuchangia harusi, au kutumia fedha zetu kwa  sherehe na anasa nyingine,  na  si kuchangia masuala ya maendeleo kama vile  elimu, afya au upatikanaji wa  maji safi na salama.

Ajabu kuna hata baadhi ya viongozi wetu wanaoona fahari na heshima kuwa wageni rasmi wakati misaada kutoka nje  inapokuja  nchini. Viongozi hawa wa wananchi watakwenda  kwenye shughuli ya kukabidhiwa , mathalan, msaada wa shilingi milioni kumi kwa ujenzi wa madarasa ya shule ya msingi ili hali wakiwa wamepanda magari ya anasa na ya gharama kubwa. Huu ni ulimbukeki wa kitaifa, maana, katika hali hiyo, hata hao  wanaotoa misaada aghalabu hawana uwezo wa kununua magari  ya  anasa ya aina hiyo.

Juhudi za mtoto Lukeman Carter zitukumbushe wajibu wetu wa kuchangia maendeleo yetu popote tulipo.  Zinakumbusha wajibu wao kwa umma, viongozi  wetu tuliowapa dhamana za uongozi.

Maana, kinachoonekana sasa ni kwa baadhi ya viongozi kuwa mbali na umma. Viongozi kuwa mbali na hali halisi. Hali za watoto wa kijijini Mahango , Madibira zinafanana na za watoto wengi katika nchi hii. Ni matokeo pia ya ufisadi uliotamalaki.

Leo tunasikia  baadhi ya kauli wanazotoa  viongozi zikidhihirisha umbali mkubwa ulio  kati yao na wanaowaongoza. Maana, kiongozi anayefahamu jinsi watu mitaani  na vijijini wanavyoathirika na vitendo vya ufisadi hatopata kigugumizi kukemea na kulaani ufisadi kila anapopata fursa ya kufanya hivyo.  Kamwe, hawezi kutetea vitendo vya kifisadi ikiwamo matumizi ya mamilioni ya shilingi kwenye kufanya sherehe , semina na makongamano yasiyo na tija kwa mwananchi.

 Ni kweli, kuwa hali ni ngumu kwa wananchi wengi. Ufisadi kwa maana ya rushwa kubwa ni chanzo kikuu cha hali hiyo. Rasilimali za wananchi zinatumika ovyo na kifisadi huku wananchi wakitaabika. Mikataba isiyo na maslahi kwa umma inatiwa saini kwa vile tu ina mgao ndani yake.

Tuna hata baadhi ya viongozi wenye utajiri wa ajabu kushinda hata  hao wafadhili wanaotupa misaada.  Yote hii inatokana na ubinafsi na uchoyo wa viongozi hawa. Wako tayari nchi inunue vifaa vibovu vya mamilioni ya dola za Kimarekani ili mradi wao wamehakikishiwa teni pasenti yao.

Ni viongozi hao hao, ambao miaka kumi iliyopita walikuwa ni watu wa kawaida, leo ni mabilionea kwa njia haramu. Na hata wanapotuhumiwa, basi, wanatumia fedha kuficha madhambi yao. Wanachofanya ni  hadaa kwa umma. Ionekane kuwa wanakubalika. Hatuwezi kuwa Taifa linalotegemea fadhila za wahisani. Tubadilike.



No comments: