WATU wanane wamekufa papo hapo, wengine tisa wakijeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Nyangao mkoani Lindi baada ya gari aina ya Land Rover, mali ya Halmashauri ya Mji Masasi kupata ajali katika kijiji cha Mtama wilaya ya Lindi Vijijini mkoani Lindi.
Gari hilo lenye namba za usajili STL 1615, lilikuwa linatokea Lindi ambako maofisa wa Halmashauri ya Masasi walikuwa wanashiriki katika Maonesho ya Wakulima (Nanenane) yaliyofanyika kitaifa katika Viwanja vya Ngongo, nje kidogo ya Manispaa ya Lindi.
Kutokea kwa ajali hiyo kulithibitishwa jana na Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Lindi, Renatha Mzinga aliyesema ilitokea juzi majira ya saa 11.30 jioni katika kijiji cha Mtama.
Aliwataja waliokufa kuwa ni Issa Salumu (33), Malik Selemani (24), Juma Ausi (21), Rajab Khalfan (17), Said Mchora (24) na Fadhili Mchalasi (26) ambapo watu wawili hadi sasa hawajafahamika majina yao, na amesema chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi.
Marehemu wote ni wakazi wa kijiji cha Mtama. Kwa mujibu wa Kamanda Mzinga, waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo ni dereva wa gari hilo, Kessy Mwaijande (40).
Pia wamo madiwani watano wa Halmashauri ya Mji Masasi ambao ni Habiba Amlima, Maimuna Chiputa, Exaveria Mhagama, Asha Abbas na Blandina Nakajumo.
Wengine ni Abraham Mohammed, Shaabani Issa Kitemwe na Ally Adam, wote wakazi wa kijiji cha Mtama.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mashuhuda wa ajali hiyo walisema kuwa majira ya jioni kwenye eneo hilo la tukio, waliliona gari hilo likiwa kwenye mwendo kasi, mazingira ambayo yalisababisha dereva wa gari hilo aliyekuwa akijaribu kukwepa mbuzi waliokuwa barabarani kushindwa kumiliki gari hilo na hatimaye kuacha njia na kuwagonga watu waliokuwa pembezoni mwa barabara hiyo, waliokuwa wakifanya biashara ndogo.
Hata hivyo, mmoja wa mashuhuda hao, Ahmad Mbonde alisema kuwa, kama si kuwakwepa mbuzi, dereva wa gari hilo asingesababisha ajali.
Kutokana na tukio hilo, Kamanda Mzinga amewataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kunusuru maisha ya watu wanaoendelea kupoteza maisha na huku wengine wakibaki na ulemavu, mazingira ambayo hupunguza nguvu kazi ya Taifa
No comments:
Post a Comment