Makusanyo ya Halmashauri Nchini Yaongezeka kwa 800% Baada ya Kuanza Kutumia Mfumo wa Kielektroniki Kukusanya Mapato - LEKULE BLOG

Breaking

Header Ads

Friday, 22 January 2016

Makusanyo ya Halmashauri Nchini Yaongezeka kwa 800% Baada ya Kuanza Kutumia Mfumo wa Kielektroniki Kukusanya Mapato


Makusanyo ya mapato katika halmashauri nchini, yameongezeka kufikia asilimia 800 hadi 900 baada ya kuanza kutumika kwa mfumo wa kukusanya mapato kwa njia ya kielektroniki katika halmashauri 164.

Hayo yalibainishwa jana na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jaffo wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari mjini Dodoma

Jaffo alisema Serikali imesanifu na kutengeneza mfumo wa kukusanya na kutoa ankara na hati za madai kwa kodi na tozo mbalimbali katika mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuachana na utaratibu wa kukusanya mapato kwa kutumia hati zinazoandikwa kwa mkono.

Alisema tangu halmashauri kuanza kutumia mfumo wa kukusanya mapato kwa njia ya kieletroniki, makusanyo yameongezeka kwa asilimia 800 hadi 900, hali ambayo inadhihirisha ukusanyaji mapato kwa njia ya stakabadhi za kuandikwa kwa mikono fedha nyingi zilikuwa zikipotea.

Alisema msingi wa kuanzishwa kwa matumizi ya mfumo huo ni kuanzisha matumizi ya benki ya TEHAMA katika kukusanya kodi na tozo mbalimbali na kuachana na utaratibu wa kukusanya mapato hayo kwa kutumia stakabadhi za kuandikwa kwa mkono, ambao hutengeneza mianya ya wizi na ubadhirifu wa fedha.

Alisema mfumo huo umekusudia kurahisisha utoaji wa stakabadhi na utunzaji kumbukumbu na kudhibiti upotevu wa mapato katika vyombo vinavyokusanya fedha za umma. 
Alisema serikali iliagiza ifikapo Julai 1, 2015, halmashauri zote ziwe zimeanza matumizi ya ukusanyaji wa mapato kwa mfumo wa kielektroniki, lakini ilipofika tarehe hiyo halmashauri 51 sawa na asilimia 28.18 ya halmashauri zote nchini, ndizo zilikuwa zimetekeleza agizo hilo.

Aidha, hadi mwanzoni mwa Desemba 2015 ni halmashauri 86 pekee sawa na asilimia 47.78 ndizo zilikuwa zimeingia katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa agizo la serikali licha ya kupewa muda hadi Desemba 31, 2015.

Alisema kutokana na kusuasua kwa zoezi hilo la serikali, ndipo agizo la msisitizo lilitolewa na Ofisi ya Rais Tamisemi kuwa ifikapo Januari 10, mwaka huu halmashauri zote ziwe zimeingia katika mfumo huo; hivyo hadi Januari 12, halmashauri 164 sawa na asilimia 90.6 zimeingia katika hatua mbalimbali za ufungaji na matumizi ya mfumo.


Pia halmashauri 17 mpya sawa na asilimia 9.4, hazijaanza mchakato wa kufunga mfumo kwa sababu mbalimbali, zikiwemo kutokuwa na ofisi ya kudumu, kutofikiwa na Mkongo wa Taifa, umeme na zingine hazijagawana mali na halmashauri mama. Alizitaka zijipange kufunga mfumo huo.
Post a Comment