Wanafunzi wa UDOM Ambao ni Wafuasi wa Chadema Watishia Kuandamana - LEKULE

Breaking

8 Mar 2016

Wanafunzi wa UDOM Ambao ni Wafuasi wa Chadema Watishia Kuandamana

Umoja  wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chaso), wametishia kufanya maandamano ikiwa Chuo Kikuu Cha Dodoma (UDOM), hakitamrejesha chuoni hapo mwanafunzi wa chuo hicho, Victor Byemelwa, aliyemsimamishwa  kwa kile  wanachodai ni sababu za  kisiasa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaama jana, Mwenyekiti wa Umoja huo, Jafary Ndege, alisema wanataka chuo hicho kimrejesha masomoni haraka na kwamba ikiwa hawatafanya, hivyo wataandamana kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma kushinikiza arudishwe.

“Tunawataka viongozi wa chuo hicho kumrejesha shuleni mwanafunzi huyo na kama wataendelea kukaa kimya tutafanya maandamano makubwa ya kushinikiza chuo hicho kimrudishe masomoni mwenzetu na yataanzia  Dar es Salaam kwenda Dodoma katika siku ambayo tutatoa taarifa kwenye vyombo vya habari iwapo ombi letu litapuuzwa,”alisema mwenyekiti huyo.

Ndege aliitaka serikali kutoa onyo kwa wanasiasa na kuacha kuingilia utendaji wa vyuo vikuu kama ilivyotokea kwa chuo hicho na kusababisha kufukuzwa mwanafunzi huyo kupitia kwa mshauri wa wanafunzi kwa barua yenye kumbukumu no Re.UDOM/DOS/36 ya Februari 5, 2016.

Kuhusu, suala la kufutiwa usajili kwa vyuo vishiriki vya  St. Joseph Songea na Arusha, na baadhi ya vitivo katika Chuo Kikuu cha Kampala Dar es Salaam, alisema wameshangazwa na hatua hiyo iliyochukuliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kwa kuwa imechangia kwa kiwango kikubwa kurudisha nyuma maendeleo ya wanafunzi wa vyuo hivyo.

Alisema kama TCU ilikuwa inafahamu kwamba havikuwa vimekidhi vigezo ni vema isingevipa usajili kuliko usumbufu unaotokea kwa wanafunzi hao hivi sasa.

No comments: