Hatimaye
vigogo 11 wa Kampuni ya Reli (TRL) waliosimamishwa kazi hapo awali
wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
wakishtakiwa na makosa tisa yakiwemo matumizi mabaya ya madaraka
yaliyopelekea manunuzi ya mabehewa mabovu 25 kinyume na utaratibu.
Washtakiwa
hao ni pamoja na Kipallo Aman Kisamfu (Mtendaji Mkuu), Jasper Hurbert
Kisiraga (Mkurugenzi Mkuu wa Ndani), Ngoso Joseph Ngosomwiles (Mhandisi
Mkuu wa Mitambo), na Mathias Andrew Massae.
Wengine
ni pamoja na Muungano Kaupunda, Paschal Mafikiri, Kedmon Mapunda, Felix
Kashaigili, Lowland Simtengu, Joseph Syaizyagi, na Charles Ndege.
Akiwasomea
mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Emillius Mchauru, Mwendesha mashtaka wa
TAKUKURU, Maxilmillian Ari amesema washtakiwa walitenda makosa hayoa
kati Januari 1, 2013 na Mei 31, 2014.
Maximillian
alisema mshtakiwa wa kwanza Kipallo Kisamfu akiwa kama Mtendaji Mkuu
alitumia vibaya madaraka yake kwa makusudi kwa kushindwa kuhakikisha
mkataba wa tenda no. PA/113/2012-13/ME/G/OE/013 unatekelezwa kwa mujibu
vigezo na masharti ya utoaji tenda na kukiuka kifungu cha 33(k) na 44(1)
na (3) cha Sheria ya Manunuzi na kusababisha Kampuni ya M/S Hindustan
Engineering and Industries Ltd kujinufaisha kutokana na mkataba huo.
Ilidawa
pia kuwa mshtakiwa namba 6, Paschal Mafikiri akiwa kama Injinia Mkuu
alitumia vibaya nafasi yake kwa kupitisha michoro na dizaini za mabehewa
aina ya Ballast Hopper Bogie Wagons (BHB) iliyoandaliwa na Kampuni ya
M/S Hindustan Ltd ambazo zilikuwa kinyume na vigezo na masharti ya
mkataba katika tenda tajwa.
Mwendesha
mashtaka wa TAKUKURU aliiambia mahakama kuwa washtakiwa wa pili na wa
tatu (Jasper Kisanga na Mathias Massae), wakiwa kama Mhasibu Mkuu na
Mhandisi Mkuu wa TRL, walitumia vibaya nafasi zao kwa makusudi kwa
kuidhinisha malipo ya kiasi cha Dola za Marekani 1,280,593.75 kwenda
Kampuni ya M/S Hindustan Ltd bila ya kuthibitisha ufanisi wa mabehewa 25
aina ya Ballast Hopper Bogie Wagons ndani ya muda wa uangalizi
(warranty period), kinyume na Sheria ya Manunuzi.
Vilevile
mshtakiwa wa 4, Muungano Kaupunda, akiwa kama Fundi Mkuu wa TRL
alitumia vibaya nafasi yake kwa kuruhusu Kampuni ya M/S Hindustan Ltd
kuanza utengenezaji wa mabehewa hayo 25 bila ya kujiridhisha kama vigezo
na masharti vya utolewaji wa tenda hiyo vilifatwa kama inavyoainishwa
na Sheria.
Kwa
mujibu wa mwendesha mashtaka, washtakiwa wa 4,7,8,9 na 10 kama wajumbe
wa kamati ya uthibitisho na huku wakijua wanatenda kosa walitumia vibaya
nafasi zao kwa kushauri na kupendekeza Kampuni ya M/S Hindustan Ltd
kushinda tenda tajwa kinyume na Sheria ya Manunuzi.
Washtakiwa
wote walikana mashtaka yao na mshtakiwa 3, 4, na 11 walifanikiwa kupata
dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wa kuaminika
watatu watakaosaini dhamana ya Shilingi Milioni Kumi kila mmoja ikiwa ni
pamoja na kuwasilisha hati zao za kusafiria mahakamani.
Washtakiwa
wengine 8 walirudishwa rumande kwa kushindwa masharti ya dhamana huku
wengine wakiwa hawana wadhamini kabisa hadi hapo kesi yao itakapotajwa
tena Februari 25, mwaka huu.
Machi
21, 2013, TRL iliingia mkataba wa kununua mabehewa hayo aina ya
Ballista Hopper Bogie (BHB) kutoka Kampuni ya M/S Hingustan Engineering
and Industrial Limited ya nchini India kwa ajili ya kutumika katika
uimarishaji wa njia za Reli ya Kati na yaliwasili Julai, 2014.
Hata
hivyo, baada ya kuanza kazi yalilalamikiwa kuwa hayakuwa na ubora
unaotakiwa na aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Dkt. Harrison Mwakyembe
aliunda kamati kwa ajili ya kuchunguza tuhuma hizo na kamati hiyo
ilikabidhi ripoti yake Desemba 1, 2014 na Waziri huyo kuahidi
kuishughulikia bodi ya zabuni ya TRL.
No comments:
Post a Comment