TUNDU Lissu, Mwanasheria wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) pia Mbunge wa Singida Magharibi leo jijini Dar es Salaam amehojiwa na Jeshi la Polisi kuhusu hoja alizozitoa kwenye Gazeti la MAWIO.
Lissu amehojiwa kwa zaidi ya saa moja Makao Makuu ya Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam baada ya kuhitajika kutoa maelezo kwa madai ya kutoa kauli za uchoelezwa zilizoandikwa kwenye Gazeti la MAWIO zilizohusu mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar.
Habari iliyoandikwa na gazeti hilo iliyobeba kichwa cha habari ‘Machafuko yaja Zanzibar’ inaelezwa kuwa sababu ya serikali kulifungia gazeti hilo tarehe 15 Januari mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza kutoa maelezo Lissu amesema, serikali inajaribu kumziba mdomo asizungumzie kuhusu suluhu ya mgogoro wa kisiasa unaoendelea visiwani Zanzibar wakati wahusika hawazingatii misingi ya demokrasia.
“Wale waliobebwa kwenye uchaguzi leo wanataka kutufumba midomo tusizungumzie masula ya uchaguzi wa Zanzibar kwani machafuko yanaweza kutokea visiwani humo kwa tahadhari hiyo wanatuita wachochezi,” amesema Lissu.
Amesema kuwa, wao wametoa tahadhari ili yasitokee machafuko na umwagikaji wa damu na kwamba, Rais John Magufuli atawajibika kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) kama alivyowajibishwa Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya.
Amesema, mahojiano yake na Gazeti la Mawio ndio yaliyosababisha yeye kuitwa na kuhojiwa na polisi na kwamba, mtazamo wake ulioandikwa kwenye gazeti hilo ndio umechangia kufutwa kwa gazeti hilo.
Amesema kuwa hatokubali kuzibwa mdomo hata kama watatumia nguvu ya polisi.
Amesema, hatua ya Rais Magufuli kukakataa kujihusisha na mgogoro wa Zanzibar haikubaliki kwa kuwa ndiye ndiye atakayepeleka jeshi pale vurugu zitakapotokea.
Lissu amefika polisi hapo akiwa na mawakili wa watatu wa Chadema ambao ni Peter Kibatala, Fedrick Kiwelo na Hekima Mwasibu.
Amesema, baada ya mahojiano hayo polisi watapeleka jalada lake kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kwa hatua zaidi.
No comments:
Post a Comment