IMG_2081
Kaimu kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida, ACP Simon Haule, akitoa taarifa ya ajali la basi la kampuni Mohammed Trans kuuwa utingo wake Abdallah Athumani  (35) mkazi wa Shinyanga mjini.

BASI  la kampuni ya Mohammed Trans aina ya scania T.858.AWY  lililokuwa likitokea jijini Mwanza likielekea jijini Dar-es-salaam,limepata ajali na kusababisha kifo cha utingo wake na kujeruhi  vibaya abiria wanne.
Utingo huyo aliyefia hospitali ya wilaya ya Iramba akipatiwa matibabu,ni Abdallah Athuman  (35) mkazi wa Shinyanga mjini.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo, Kaimu kamanda wa jeshi la polisi mkoani Singida, ACP Simon Haule, alisema ajali hiyo imetokea Januari 9 mwaka huu saa 6.45 mchana huko katika mlima Sekenke wilaya ya Iramba.
Alisema siku ya tukio basi hilo lililokuwa likiendeshwa na Jovin Jonson (35) lilipofika eneo la tukio,liligonga kingo za daraja na kusababisha kifo cha utingo na abiria wengine wanne kujeruhiwa.
Haule alitaja waliojeruhiwa kuwa ni mkazi wa Kahama mkoani Shinyanga Asha Said (20) mkaguzi wa ndani wa mahesabu wa kampuni ya Mohammed ambaye amekatika mguu wa kushoto.
“Mkulima na mkazi wa Tengo wilaya ya Kahama,Lucas Deo (22) amevunjika miguu yote miwili na wote wawili na mwenzake Asha,wamehamishiwa hospitali ya rufaa Bungando jijini Mwanza kwa matibabu zaidi”,alisema kaimu kamanda huyo.
Haule allisema Felix Matimati (30) mkazi wa Shinyanga mjini,yeye ameteguka mguu wa kushoto na amepatiwa matibabu ya kuruhusiwa,wakati Alafati Said (24) mkazi wa jijini Mwanza,amepata majeraha mguu wa kushoto,ametibiwa na kuruhusiwa.
Kaimu kamanda huyo,alisema chanzo cha ajali hiyo ni hitilafu ya usukani wa basi hilo na hivyo kupelekea dereva Jovin kushindwa kulimudu.Dereva huyo hivi sasa anashikiliwa na polisi.