Rais wa
China Xi Jinping amewaambia viongozi wa Afrika, nchi yake itatoa dola
bilioni 60 kufadhili miradi ya maendeleo barani Afrika. Xi ameyasema
hayo katika mkutano wa kilele wa ushirikiano kati ya China na Afrika.
Xi,
anayeuongoza mkutano huo ameorodhesha mpango wa maendeleo wa maendeleo
wenye vipengee kumi wa taifa lake barani Afrika akisema anataka kujenga
uhusiano wa haki na washirika walio sawa.
"Katika
kuhakikisha utekelezwaji wa hatua hizi 10 za ushirikiano, China imeamua
kutoa dola bilioni 60 ya kuendeleza miradi hiyo," alisema Xi katika
mkutano huo unaofanyika mjini Johannesburn Afrika Kusini.
Hatua
hizi zinanuiwa kuangazia mambo matatu yanayoaminika kuirejesha Afrika
nyuma kimaendeleo, ambayo ni masuala ya, miundo mbinu, ukosefu wa
wataalamu walio na ujuzi mbali mbali na ukosefu wa fedha za kuendeleza
miradi hiyo.
Xi
Jinping ameongeza kwamba fedha zitakazotolewa zitajumuisha dola bilioni
tano ya mikopo isiyokuwa na riba na dola bilioni 35 ya mikopo ilio na
mashrti nafuu itakayotolewa kwa Afrika. Katika hotuba yake ya ufunguzi
kwenye mkutano huo, Xi pia alitangaza msaada wa kupambana na ukame
barani Afrika.
"China
ina wasiwasi mkubwa juu ya mavuno duni yaliosababishwa na mvua ya El
Nino katika mataifa mengi ya Afrika na itatoa dola milioni 156 ya
kushughulikia msaada wa vyakula vya dharura katika maeneo
yatakayoathirika," alisema Xi Jinping.
China kuwekeza zaidi barani Afrika
Kando na
uchumi wa china kupungua au kukuwa kwa kasi ndogo, na kusababisha
Beijing kukatiza uwekezaji wake Afrika kwa zaidi ya asilimia 40 katika
miezi sita ya mwanzo ya mwaka huu wa 2015, Xi amesema china itaimarisha
hatua za uwekezaji katika viwanda vinavyotengeneza chakula kwaajili ya
soko la nje, pamoja na kujenga barabara, bandari na reli, katika bara la
Afrika linaloonekana kuwa na soko kubwa kutoka China.
Rais huyo
wa China amesema nchi yake pia itaimarisha ushirikiano wake barani
Afrika katika vita vyake dhidi ya makundi yalio na itikadi kali na
imesema haitoingilia michakato ya kiasiasa ya serikali za bara hilo.
Afrika
kwa ujumla inaiona China kama mpambanaji mzuri kuliko ushawishi wa
Magharibi, japokuwa mataifa hayo ya Magharibi yanaishutumu China kwa
kufumbia macho migogoro na ukiukwaji wa haki za binaadamu unaofanyika
barani Afrika wakati wanapojiingiza barani humo kibiashara.
Mkutano
huo wa siku mbili wa ushirikiano kati ya China na Afrika ni wa pili
kufanyika ambapo China inawakusanya pamoja viongozi wa Afrika tangu
kuzinduliwa kwake mjini Beijing mwaka wa 2000.
Tangu wakati huo biashara ya China Barani Afrika imeipiku ile ya washirika wake wa Ulaya na Marekani
Mwandishi: Amina Abubakar/ Reuters, AFP,
Mhariri: Josephat Charo
Chanzo:DW
No comments:
Post a Comment