17 Nov 2015

VIONGOZI WIZARA YA NISHATI NA MADINI WAFANYA ZIARA LINDI NA MTWARA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Omar Chambo na Naibu wake, Mhandisi Paul Masanja pamoja na Kamishna wa Nishati, Mhandisi Hosea Mbise hapo jana walifanya ziara kwenye maeneo mbalimbali yanayopitiwa na mradi mkubwa wa Gesi Asilia.

Lengo kuu la ziara hiyo ni kujionea shughuli zinazoendelea kwenye mradi wa gesi asilia pamoja na kuzungumza na wafanyakazi wa maeneo hayo kuhusu masuala mbalimbali ya shughuli zao za kila siku.

Maeneo ambayo yalitembelewa na viongozi hao ni pamoja na Kituo cha Kupokea Gesi Asilia ya Mtwara na Lindi cha Somangafungu (Somangafungu Gas Receiving Station) kilichopo wilayani Kilwa, mkoa wa Lindi; Visima vya gesi asilia vya Mnazi Bay na Msimbati; Sehemu iliyoathiriwa na Mmomonyoko wa ardhi ya Msimbati na Kituo cha Kuchakata gesi asilia cha Madimba cha mkoani Mtwara.

Wengine katika ziara hiyo ni Kamishna Msaidizi wa Nishati sehemu ya Gesi Asilia, Mhandisi Norbert Kahyoza, Meneja wa Kampuni ya Gesi Asilia (GASCO), Mhandisi Kapuulya Musomba na Maafisa kutoka Wizara ya Nishati na Madini.

Ziara hiyo ni miongoni mwa mikakati iliyowekwa na viongozi hao kukagua shughuli mbalimbali za masuala ya Nishati na Madini kote nchini.
Baadhi ya mitambo katika Kituo cha Kupokelea Gesi Asilia kutoka Songosongo na Mtwara kilichopo Somangafungu wilayani Kilwa Mkoani Lindi
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Omar Chambo (kulia) na Naibu wake, Mhandisi Paul Masanja (kushoto) wakimsikiliza Meneja wa Kampuni ya GASCO, Mhandisi Kapuulya Musomba (hayupo pichani) akiwaeleza kuhusu Kituo cha Kupokelea Gesi cha Somangafungu. Katikati ni Msimamizi wa Kituo hicho, Mhandisi Msafiri Peter.
Baadhi ya mitambo ya kupokelea gesi asilia iliyopo kwenye maeneo kilipo kisima cha gesi asilia cha Mnazi Bay Namba 3.
Sehemu ya Mitambo ya kuchakata gesi asilia ya Madimba inavyoonekana wakati wa usiku. Kituo hicho cha Madimba kilitembelewa na viongozi hao na kujionea shughuli zinazoendelea kituoni hapo.
Sehemu ya eneo lililokumbwa na Mmomoyoko wa ardhi uliotokea Mwezi Januari mwaka huu katika kijiji cha Msimbati baada ya mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali kunyesha katika maeneo hayo. Katika eneo hilo bomba kubwa la gesi asilia linakatiza kuelekea kwenye kituo cha kuchakata gesi asilia cha Madimba.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Omar Chambo (wa sita kutoka kushoto) na Naibu wake, Mhandisi Paul Masanja (kushoto kwake) wakiwa katika picha ya pamoja na wataalamu wengine mara baada ya kutembelea kisima cha gesi asilia cha Mnazi Bay namba 3 (MB 3). 

No comments:

Post a Comment