15 Nov 2015

Uchaguzi Mkuu Zanzibar Wavunja Ndoa 4


Athari  za uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, zimeanza kujitokeza Zanzibar ambapo jumla ya wanawake wanane wamepoteza ndoa zao baada ya kulazimishwa kupiga kura kinyume na matakwa yao, kinyume na demokrasia ya mfumo wa vyama vingi.

Wakizungumza na mtandao huu wanawake hao walidai kwamba wamepewa talaka na waume zao ambao walikuwa wanataka pamoja na kuwalazimisha kufahamu wanakweda kumpigia mgombea gani ambaye wakati wa uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Oktoba ambao ulifutwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar(ZEC).

Mkazi wa Kijiji cha Kandwi, mkoa wa Kaskazini, Jimbo la uchaguzi la Nungwi Unguja Tatu Mkombe alisema alikatazwa na mume asiende kupiga kura kwa sababu kura yake inaweza kusababisha fitina kubwa katika nchi.

“Mimi ni mfuasi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) na mume wangu anatoka Chama cha Wananchi (CUF), alinikataza nisiende kupiga kura kwa madai kwamba kura yangu inaweza kusababisha fitina kubwa katika nchi hii, lakini nilipomuuliza fitina gani alishindwa kuniambia,” alisema na kuongeza kuwa alipinga uamuzi huo na alikwenda kupiga kura na ndipo aliporudi alikuta tayari talaka yake imewekwa katika kabati na kukabidhiwa.

Hata hivyo, Tatu alisema amepokea ombi la mumewe akimtaka warudiane na kwamba na yeye amekubaliana na maamuzi hayo ingawa kwa shingo upande zaidi kwa ajili ya kulinda matunzo ya watoto wake wanaofikia sita ambapo katika kipindi cha wiki mbili walichotengana malezi yote yalikuwa juu yake.

“Nimeamua kurudi kwa mume wangu sina ujanja kwa sababu malezi yote ya watoto katika kipindi cha wiki mbili yameniangukia mimi huku mume wangu hana habari na jambo lolote,” alisema.

Salma Ibrahim Sultani (40), mkazi wa Kivunge alisema talaka aliyopewa sasa ni ya pili ambapo awali alipewa katika kipindi cha uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura na mumewe kwa kumshutumu kuleta ndugu zake kuandikishwa katika jimbo la Mkwajuni ili kuiunga mkono CCM.

Alisema mara baada ya kupewa talaka ya pili amechukua uamuzi na kusema kamwe hawezi kurudi tena katika ndoa yake hiyo kwani hawezi kuishi kwa shinikizo la kisiasa. 
 
Mratibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) Zanzibar, Mzuri Issa alikiri kupokea taarifa hizo zinazohusu matukio ya udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake dhidi ya waume zao, ikiwemo utoaji wa talaka kutokana na tofauti za kisiasa.


Akifafanua zaidi Mzuri alisema Tamwa kupitia watendaji wake wameanza kulifanyia kazi suala hilo kwa kina kufahamu ukweli wake ukoje.
 
 Mke wa Makamu wa Pili wa Rais, Mama Asha Suleiman ameeleza kusikitishwa na tabia hiyo iliyofanywa na baadhi ya wanaume ambao wamesahau ubinadamu na kuweka mbele tofauti za itikadi za kisiasa.

No comments:

Post a Comment