11 Nov 2015

TEWUTA wampongeza Rais Dk. Magufuli, wamuomba kugeukia mashirika ya mawasiliano ya Serikalini

tewuta
Katibu mkuu wa TEWUTA, Junus Ndaro (katikati) alkizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) mapema leo jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mwenyekiti wa TEWUTA, Pius Makuke, kushoto ni afisa kutoka chama hicho. 
Na Rabi Hume
[DAR ES SALAAM] Chama cha Wafanyakazi wa Sekta ya Huduma za Mtandao wa Mawasiliano Tanzania (TEWUTA), kimemtaka rais wa Tanzania, Dr. John Magufuli kuyasaidia mashirika ya mawasiliano yaliyo chini ya seikali kutokana na mashirika hayo kuwa na hali mbaya ya utoaji huduma na mfumo mzima wa manejimenti zake.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Habari Maelezo, Katibu Mkuu wa Tewuta, Junus Ndaro alisema mashirika ya mawasiliano yaliyochini ya serikali ya Posta na TTCL yamekuwa yakizidi kuwa na hali mbaya na mtu pekee anayeweza kuyaokoa ni rais.
Ndaro amesema kuwa mashirika yaliyochini ya serikali ya Posta na TTCL yamekuwa na changamoto nyingi ambazo zimekuwa zikichochewa na viongozi wanaoongoza mashirika hayo na kuhitaji rais kuingilia jambo hilo ili kuyasaidia mashirika hayo yarudi kama awali.
“Sisi kama TEWUTA tunamtaka rais Magufuli kwa kutumia kauli yake ya hapa kazi tu basi na hizi sekta za mawasiliano aweze kuyasaidia mashirika hayo ambayo kwa sasa yapo katika hali mbaya,” alisema Ndaro.
Katibu Mkuu huyo ametolea mfano Shirika la Simu Tanzania (TTCL) kuwa limekuwa na utendaji mbovu wa kazi na kuwatupia lawama viongozi wa shirika hilo kwa kuwa na tabia ya kujilipa mishahara mara mbili kwa mwezi na kupeana fedha ya nauli kila mwezi 600,000 huku wafanyakazi wa kawaida wakiwapa 42,000 pekee.
Aidha kupitia mkutano huo na waandishi wa habari, Ndaro ametumia fulsa hiyo kuzungumza kwa niaba ya TEWUTA aina ya Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia ambae wanadhani atakuwa mtu sahihi kutatua matatizo ambayo yatakuwa yanatokea ndani ya sekta hiyo kuwa anatakiwa kuwa mzalendo kwa kufanya kazi kwa kujua kwamba anasaidia nchi yake.
Sifa nyingine ambayo amesema waziri huyo anapaswa kuwa nayo ni kuwa mchapa kazi na kuwa tayari kufanya kazi muda wowote ambao atahitajika kufanya kazi na asiwe anamiliki hisa katika shirika lolote la mawasiliano kwa sababu akiwa mtu ambaye ana hisa atapendelea mashirika yasiyo ya serikali.
“Chama cha Wafanyakazi cha TEWUTA tunawasilisha ombi rasmi kwake, kuwa iwapo ataunda Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kwa faida ya sekta ya mawasiliano tunaomba achague kiongozi ambaye ni mzalendo na mchapakazi ili aje kufanya kazi ya kutatuua changamoto hizi,
“Sifa nyingine lazima asiwe na hisa katika kampuni yeyote ya mawasiliano, tukiwa na kiongozi mwenye hisa kwenye makampuni mengine hatakuwa akiyasimamia vyema mashirika ya serikali badala yake ataangalia makapuni binfasi,” alisema Ndaro.
Pamoja na hayo pia wametoa mapendekezo yake kwa rais ambayo ni pamoja na kuteua wajumbe wapya wa bodi ya wakurugenzi wakiamini kuwa wajumbe hao ndiyo wamekuwa wakishinikiza shirika hilo kuwa kufanya mambo ambayo ni kinyume na taratibu licha ya kuwa na Mwenyekiti mpya Bw. Tolly Mbwete ambaye hawezi kufanya maamuzi pekee bila wajumbe kuridhia.
Pendekezo lingine ambalo wamelitoa kwa rais Magufuli ni kuifukuza kampuni ya RubieM ambayo kwa mujibu wa TTCL ilikuja Tanzania mwaka 2013 kwa mkataba wa miezi sita (6) kwa ajili ya kuwa wanatoa ushauri kwa shirika jinsi ya kufanya biashara kisasa lakini wamekuwa wakifanya kazi hadi sasa na kwa maelezo ya Tewuta wamefanya uchunguzi na kugundua kampuni hiyo ina kashfa nyingi za ufisadi na kuamini yawezekana kuna ufisadi unaofanyika kwenye shirika la TTCL.
Mambo mengine ya kawaida ambayo wamemuomba rais ni pamoja na kupunguza kodi kwa wafanyakazi, kuitaka TTCL kupunguza tozo ya kuunganisha simu (interconnection cherge) ili kuwapatia unafuu wananchi wa kawaida kuweza kufurahia huduma kutoka kwa shirika la simu.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Taifa wa TEWUTA, Pius Makuke amesema wamefikia hatua ya kuweka wazi mambo hayo kutokana na mambo kuzidi kuwa mabaya na walizungumza na uongozi wa TTCL lakini hakuna hatua waliyochukua na sasa wanafata kwa rais kama na yeye hatochukua hatua yeyote basi watakwenda mahakamani.

No comments:

Post a Comment