14 Nov 2015

Kijana Aliyesambaza Taarifa Za Mkuu wa Majeshi Kulishwa Sumu Akwama tena Kupata Dhamana

Mwanafunzi wa Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT), Benedict Ngonyani anayekabiliwa na kesi ya kusambaza taarifa za uongo kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange amelishwa sumu na kupelekwa nchini Kenya kwa matibabu anaendelea kusota rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu Respicius Mwijage jana alimpa masharti mshtakiwa huyo ya kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika, kila mmoja asaini bondi ya Sh5 milioni.

Vilevile, alisema wadhamini hao wanatakiwa kuwa na barua zinazotambulika.

Mshtakiwa huyo alishindwa kutimiza masharti hayo na kurudishwa rumande hadi Novemba 25. Upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea.

Awali Wakili wa Serikali, Shedrack Kimaro kwa kushirikiana na Mwanasheria Mwandamizi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Johannes Kalungula walidai kuwa mshtakiwa huyo alisambaza taarifa hizo za uongo kupitia mtandao ya kijamii ukiwamo wa WhatsApp na Facebook kinyume na Kifungu cha 16 cha Sheria ya Mtandao Namba 14 ya Mwaka 2015.

Wakili Kimaro alidai kuwa Septemba 25 jijini Dar es Salaam, mshtakiwa huyo alisambaza taarifa hizo kwa lengo la kupotosha umma.

Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) aliwasilisha mahakamani hapo hati ya kuzuia dhamana ya mshtakiwa huyo akidai kuwa ni masilahi na Taifa.


Mwanafunzi huyo ni mshtakiwa wa kwanza kufikishwa mahakamani na kufunguliwa mashtaka kupitia Sheria mpya ya Makosa ya Mtandaoni.

No comments:

Post a Comment