15 Nov 2015

Halmashauri Zakumbushwa Shule Kuachana na Michango


HALMASHAURI za jiji la Dar es Salaam zimetakiwa kutenga fungu ili kusaidia kupunguza michango mashuleni na kuendana na agizo lililotolewa na rais kuhusu elimu kutolewa bure kuanzia mwaka 2016.

Akizungumza juzi jijini Dar es Salaam Katibu Mkuu katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Jumanne Sagini alisema ni jukumu la kila halmashauri kusaidia shule zilizopo katika maeneo yao ili kupunguza michango kwa wazazi.

Alisema manispaa nyingi zinakusanya kodi mapato ya kodi yanayotokana na michango ya wananchi na yamekuwa yakiongezeka hivyo ni vyema wakurugenzi wakatumia busara kutekeleza agizo la Rais John Magufuli kwa kutoa kiasi cha fedha kununua madawati, kujenga madarasa na kumlipa mlinzi pamoja na michango mingine.

“Najua mnapata fedha nyingi tu tumieni kiasi kidogo kulipia ulinzi wa shule na michango mingine tuondoe hii kero kwa wazazi na kuendana na agizo la rais,” alisema Sagini. 
 
Aidha alisema aina ya michango ambayo kamati zitaamua isiwe ya kumfukuzisha mwanafunzi shule au kumtoa katika masomo ya ziada ‘tuition’ zisilazimishwe kwa kuwa walimu wanalipwa mishahara na serikali ili wafundishe.


Alisema kwa mtendaji yeyote atakayekwenda kinyume na agizo kazi itakuwa imemshinda na ataondolewa mapema na kuna baadhi ya shule za Dar es Salaam zimelalamikiwa kuanza kutoza michango kwa wazazi kinyume cha sheria ya elimu.

No comments:

Post a Comment