Wabunge wanaounga umoja wa Katiba Ya Wananchi, UKAWA wametolewa nje ya ukumbi wa bunge muda huu baada ya kugoma kutambua ujio wa Dr Shein bungeni na kuanza kuzomea huku wakisema Maalim Seif....Maalim Seif
Wabunge hao awali walitoa msimamo wao wa kutokubali Dk Ali Shein kuhudhuria Bunge hilo wakati rais atakapoingia Bungeni kulihutubia Bunge kwa kuwa hawamtambui kama rais wa Zanzibar kwani kwa mujibu wa Katiba muda wake umekwisha.
Kelele za zomeazomea ziliibuka ghafla wakati Rais Dk Shein alipoingia bungeni hali iliyoondoa utulivu wa Bunge.
Hata hivyo, Mbunge pekee wa upinzani, Zitto Kabwe (ACT – Wazalendo) alibaki ndani ya Bunge kwa utulivu na kuendelea kusikiliza hotuba ya Rais.
Awali, wabunge hao walimuandikia barua Spika wa Bunge wakihoji uhalali wa hotuba ya Rais bungeni endapo Dk Shein atahudhuria Bunge hilo kama Rais wa Zanzibar.
Ukawa wameendelea kushinikiza Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Zanzibar (NEC) kumtangaza mshindi wa nafasi ya Urais wa Zanzibar, huku mgombea wa CUF Maalim Seif Sharif Hamadi akidai kuwa ameshinda kutokana na kura halali alizokusanya kwenye vituo vyote.
Spika wa bunge,Job Ndugai aliwataka wabunge hao waache kuzomea na badala yake wakae chini lakini wakakaida, hali iliyomfanya awaamuru watoke nje kwa hiari yao kabla nguvu ya dola haijatumika kuwatoa.
No comments:
Post a Comment