Biashara ya Maduka ya Dawa Baridi Muhimbili Yavurugwa - LEKULE

Breaking

28 Nov 2015

Biashara ya Maduka ya Dawa Baridi Muhimbili Yavurugwa

BIASHARA ya maduka ya dawa baridi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili imeingia shubiri, huku maduka mengine katika hospitali za Serikali yakitakiwa kuwa tayari baada ya agizo la Rais John Magufuli, kuanza kutekelezwa.
 
 Dk Magufuli alipoingia madarakani tu, moja ya maagizo yake alitaka Bohari ya Dawa (MSD) kufungua maduka ya dawa za Serikali kwenye hospitali za rufaa na za kanda, ambapo kesho kutwa Jumatatu duka hilo litaanza kufanya kazi Muhimbili na bei za dawa zitakuwa chini ya bei ya soko.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laureane Bwanakunu, amesema kufunguliwa kwa duka hilo kutaenda sambamba na kufunguliwa na duka lingine katika Hospitali ya Kanda ya Mbeya na baadaye kwenye hospitali zingine za rufaa na kanda na yatatoa huduma mpaka kwa wanaotumia utaratibu wa bima ya afya.

Kwa mujibu wa Bwanakunu, pia MSD imeanza kuweka nembo ya Serikali kwenye vidonge na hadi sasa ina vidonge 45 ambavyo vimewekewa nembo ya GOT, ili kudhibiti wizi wa dawa za Serikali. 
 
Bwanakunu amesema agizo la Rais la kuitaka MSD kuanzisha maduka ya dawa karibu na hospitali hasa pale Muhimbili, limekuja wakati muafaka. 
 
Alisema kwenye mpango mkakati wa miaka sita wa MSD, walikuwa na malengo ya kufungua maduka hayo kwa ajili ya kusogeza huduma karibu kabisa na wananchi.

“Agizo la Rais limetekelezwa na duka la Muhimbili litafunguliwa Jumatatu, tunamalizia hatua zilizobaki na mafundi wanafanya kazi usiku na mchana,” alisema na kuongeza kuwa duka hilo ambalo litatumia mfumo wa risiti wa kielektroniki, tayari vibali vyake vyote vimepatikana.

Bwanakunu alisema wamefanya ziara ya kutembelea hospitali ya Benjamini Mkapa iliyopo Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na kufanya mazungumzo na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa hospitali hiyo, Profesa Gesase Peter, ambaye aliahidi kuwapa eneo kubwa kwa ajili ya kuendeshea duka hilo, litakalohudumia wateja wa Kanda ya Kati.

Mkurugenzi huyo alisisitiza kuwa maduka ya MSD ambayo yatafunguliwa kwenye hospitali za rufaa na kanda, yatafanya kazi saa 24 na kuuza dawa na vifaa tiba chini ya bei ya soko na yatahudumia watu binafsi na wale waliopo kwenye taratibu za bima za afya.

Alisema maduka hayo yataiongezea bohari wigo wa utendaji katika kutoa huduma kwa wananchi, tofauti na sasa ambapo huduma ya dawa na vifaa tiba zinatolewa kupitia mali zinazohifadhiwa katika bohari kupitia orodha ya taifa ya dawa na vifaa tiba yenye aina ya dawa na vifaa tiba takribani 3,000 zinazoingizwa kwa mahitaji maalumu.

Kuhusu udhibiti wa wizi wa dawa, Mkurugenzi huyo alisema MSD inafanya kazi za uagizaji, uhifadhi na usambazaji kwa kutumia mfumo wa mtandao wa E9.
 
 “Lakini ili kudhibiti upotevu wa dawa za Serikali tangu mwaka wa fedha uliopita tumeanza kuziwekea alama ya GOT bidhaa zetu ikiwa ni pamoja na vidonge, mkumbuke zamani ilikuwa tunaweka kwenye vifungashio vya ndani na maboksi alama ya MSD, lakini sasa hata kidonge kina alama ya GOT, pale Dar es Salaam nina sampuli ya vidonge hivyo,” alisema.

Alisema vidonge ambavyo tayari vimewekewa nembo ya GOT vipo 45 na wanaendelea kuwapa maelekezo wazabuni, ili vyote viwekwe alama hizo.
 
 Akitaja aina za dawa zenye nembo ya serikali, Mkurugenzi huyo alisema tayari dawa aina ya Diclofenac, Amoxillin, Ciprofloxacin, Contrimoxale, paracetamol na magnesium.

Pia alisema sasa wataanzisha huduma ya kutoa taarifa kwa njia ya simu ili wananchi watakapoona kuna wizi wa dawa za Serikali, watoe taarifa na wananchi wataelimishwa kutoa taarifa pale wanapoona dawa za serikali mitaani. 
 
“Dawa nyingi zinaibwa kwenye vituo ambavyo dawa zinapelekwa na sasa watatumia mfumo wa kompyuta kubaini wizi wa dawa ambazo zimekuwa zikiibwa mkoa moja na kupelekwa mkoa mwingine.

“Rais Magufuli amesema miongoni mwa vipaumbele vyake ni maji na dawa, MSD imejipanga kuokoa maisha ya Watanzania,” alisema na kuongeza kuwa bajeti ya dawa ikiongezwa na kufikia Sh bilioni 250 kila mtu atapata dawa.


Pamoja na jitihada hizo, Bwanakunu alisema bado MSD inaidai Serikali fedha nyingi ambazo alisema tayari wameanza kulipwa. “Tunaidai Serikali Sh bilioni 53 deni ambalo limehakikiwa na majuzi tumelipwa Sh bilioni 14,” alisema.

No comments: