14 Oct 2015

Mzindakaya: Waliohama CCM Wapuuzwe



MWANASIASA mkongwe nchini, Chrisant Mzindakaya amewataka viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wagombea wao wa nafasi mbalimbali, wasigombane na waliohama chama hicho kwa kusisitiza kwamba wakifanya hivyo, watakuwa wanakosea.

Mzindakaya alisema, CCM ni chama chenye heshima kubwa duniani na chenye Ilani ya Uchaguzi bora, yenye heshima. Alisisitiza kuwa rais bora wa awamu ya tano atatoka katika chama hicho.

Alisema hayo juzi akiwawakilisha wazee wa mkoa wa Rukwa kwenye mkutano wa kampeni ya kuwanadi wagombea urais, ubunge na udiwani kwa tiketi ya CCM uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Ndua, Manispaa ya Sumbawanga.

Mkutano huo wa kampeni ulihudhuriwa na Mjumbe wa Kamati Kuu CCM Taifa na Halmashauri Kuu, Mizengo Pinda ambaye pia ni Waziri Mkuu. Wengine ni pamoja na viongozi waandamizi wa CCM mkoa na wilaya.

“Sisi wazee wa mkoa huu tunasema chama cha siasa chenye heshima kubwa duniani ni CCM ambapo bila wasiwasi ndiko atakakotoka rais wa awamu ya tano ambaye ni Dk John Magufuli …Tunawaasa viongozi wa CCM na wagombea wasihangaike kugombana na wale waliohama CCM mkifanya hivyo mtakosea sana,” alisisitiza .

No comments:

Post a Comment