18 Sept 2015

Umoja wa Ulaya Watabiri mchuano Mkali Kati ya CCM na UKAWA......Watuma Mamia ya Waangalizi Watakaopiga Kambi Nchi nzima


Umoja wa Ulaya (EU), umesema Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu nchini, una ushindani mkali na siyo mwepesi kama chaguzi nne zilizopita chini ya mfumo wa vyama vingi.

Tangu kuanza kampeni za Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu, wagombea urais wanaoonekana kuchuana vikali ni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam katika kongamano la amani lililoandaliwa na Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (Moat) na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Mkuu wa Ujumbe wa EU, Balozi Filiberto Sebregondi, alisema chaguzi zilizopita jicho lao kubwa lilikuwa Zanzibar kutokana na ushindani uliokuwapo.

“Zanzibar hali ilikuwa ngumu kwa wakati ule, lakini siasa zimebadilika, uchaguzi wa sasa ni wenye ushindani mkubwa, kampeni zinazoendelea ni zenye ushindani, tuangalie joto la uchaguzi lisije kusababisha kutoweka kwa amani,” alisema.

Alisema hadi sasa EU inaridhishwa na mwenendo wa kampeni na kinachotakiwa ni kwa wagombea kuendeleza kampeni za amani, kistaarabu na kuhakikisha kila mmoja anawajibika katika nafasi yake.

Balozi Sebregondi alisema hadi sasa waangalizi wao 34 wameshaingia nchini na matarajio yao ni kuwa na waangalizi 134 katika wiki tano hadi sita kabla na baada ya uchaguzi.

Alisema chaguzi zilizopita waangalizi wa EU walielekezwa zaidi Zanzibar kutokana na hali ya kisiasa iliyokuwapo, lakini kwa sasa watasambazwa nchi nzima kutokana na hali ya kisiasa iliyopo.

“Kwa EU Uchaguzi Mkuu ni kipaumbele katika kuchangia ukuaji wa demokrasia,” alibainisha.

Kwa mujibu wa Balozi  Sebregondi, EU imeingiza kiasi cha Euro bilioni 1.2 kwa nchi za Afrika kwa ajili ya ulinzi na usalama, na kuhakikisha uwepo wa amani.

Aidha, alisema wakati wa uandikishaji wa wapigakura Zanzibar yalitokea malalamiko mengi ambayo yangeandikwa kwa kina yangesaidia kupata ufumbuzi.

Aliwataka waandishi wa habari kutumia vizuri kalamu zao kwa kuripoti mambo yenye kujenga amani pamoja na kuwakemea viongozi au wanasiasa wanaotaka kusababisha machafuko.

Naye, Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN) nchini, Alvaro Rodriguez, alisema Jumuiya ya Kimataifa inafuatilia kwa karibu uchaguzi huo ili kuisaidia Tanzania kuendelea kuvutia watalii, wawekezaji katika maendeleo na kuongeza ajira, pamoja na kuendelea kuwa mdau wa maendeleo na nchi ya kidemokrasia.

Alisema migogoro ina gharama kubwa katika jamii kwa kuwa machafuko huaribu miundombinu, kukimbiza wafanyabiashara, wawekezaji, watalii pamoja na kupoteza kuaminiana ndani ya familia.

“Jamii iliyotengwa kwa kukosa elimu, ajira na inayoishi katika maisha ya chini, wanaweza kuandaliwa au kuwa waathirika wakubwa wa uvunjifu wa amani pamoja na kuongeza ukatili kwa makundi ya wanawake na watoto."

Rodriguez alisema UN imesaidia mafunzo kwa wawezeshaji wa haki za binadamu, jinsia na nafasi ya jeshi la polisi wakati wa Uchaguzi Mkuu.

Alisema maafisa wa polisi 103 walifundishwa kwa siku tano kuhusu masuala mtambuka, haki za binadamu, jinsia, utatuzi wa migogoro, hatua za uchaguzi, kukamata na matumizi ya vyombo vya moto.

“Kubwa kinachoangaliwa kwa sasa ni nafasi ya Jeshi la Polisi wakati wa Uchaguzi Mkuu na jinsi ya kufanya kazi na vyombo vya habari,” alisema.

Alisema mafunzo hayo yatawafikia maafisa wa polisi 6,000 na kwamba matarajio ya UN ni kufanya kazi kwa utaalamu, kutoa taarifa na kuzuia ukatili hasa kwa makundi yaliyotengwa.

“Matarajio yetu ni kuwa jitihada hizi zitachangia amani na uchaguzi huru kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu kushiriki katika uchaguzi kama wagombea na wapigakura bila ukatili na unyanyasaji, na waandishi wa habari kuripoti uchaguzi katika mazingira ya amani,” alisema.

Kwa mujibu wa Rodriguez, wanashirikiana kwa karibu na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) kuzisaidia katika mchakato wa utangazaji matokeo ya uchaguzi, uwazi na kuzingatia muda kama njia ya kuzuia migogoro katika uchaguzi huo.


Aliongeza kuwa UN itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Serikali na Watanzania kwa kuzingatia maono kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu.

No comments:

Post a Comment