Na.Jumbe Ismailly
[Ikungi,
Singida]Shule ya msingi Taru namba saba iliyopo kata ya Sambaru,
tarafa na wilaya ya Ikungi, Mkoani Singida haijasajiliwa kwa kipindi cha
miaka sita sasa, hali inayochangia wanafunzi wa darasa la nne kutembea
umbali wa kilomita 22 kwenda kufanya mtihani wa kuingia darasa la dano
katika shule mama ya Sambaru.
Mwenyekiti
wa Kijiji cha Sambaru, Mfaume Hassani Masudi aliyasema hayo baada ya
kutakiwa na mtandao huu kutoa maelezo ya sababu zipi zilizochangia shule
hiyo kutosajiliwa licha ya kuwa na wanafunzi 200 wa darasa la awali
hadi darasa la tano lakini mpaka sasa bado haijasajiliwa.
Alifafanua
mwenyekiti huyo kwamba shule hiyo inayoingia mwaka wa sita sasa ina
vyumba vya madarasa matatu, nyumba moja ya mwalimu na matundu ya vyoo
imeshindikana kupata usajili kutokana na uongozi uliopita wa serikali ya
Kijiji hicho kutopeleka taarifa sahihi za kuwepo kwa shule hiyo
wilayani.
“Kwa
hiyo tatizo lililokuwepo ni kutokana na shule yetu hii ya Taru namba
saba kama inavyojulikana ni shule ambayo imeanza na sasa hivi inaingia
mwaka wa sita,wanafunzi wapo lakini shule bado haijasajiliwa huku ikiwa
na vyumba vya madarasa matatu na nyumba moja ya mwalimu”alifafanua.
“Lakini
tatizo ambalo tumeendelea kulifuatilia baada ya sisi kuingia kwenye
madaraka ndiyo hilo ambavyo tulivyosema kwamba taarifa tumeambiwa
hazijapelekwa kule wilayani kwamba kuna shule inatakiwa
isajiliwe”alibainisha mwenyekiti huyo wa kijiji.
Hata
hivyo Masudi alisisitiza kwamba baada ya kubaini hilo utaratibu
uliofanywa na ofisi yake ni kuandaa muhtasari wa serikali ya Kijiji
hicho wanaotarajia kuupeleka kwenye kikao cha kamati ya maendeleo ya
kata hiyo (WDC),kikao ambacho hakijaitishwa na ofisa mtendaji wa kata
hiyo tangu walipochaguliwa.
Kwa
mujibu wa mwenyekiti huyo inavyoonekana shule hiyo ilianzishwa kwa
mazingira ya kisiasa baada ya wazazi kuamua kujenga shule hiyo ambayo
mbunge wa jimbo hilo, Tundu Lissu ndiye aliyekuwa akitoa misaada
mbalimbali katika shule hiyo ikiwemo kuwalipa posho walimu wanaofundisha
wanafunzi wa shule hiyo.
“Kwa
sababu shule ilianza kisiasa,wazazi waliamua wajenge shule pale kwa
hiyo na msaada ukaonekana unatolewa na mbunge sasa viongozi waliokuwepo
wa serikali ya Kijiji walikuwa wanatokana na CCM,na kwa kuwa mbunge huyo
ni wa CHADEMA hivyo hawakuona umuhimu wa kuisajili shule
hiyo”alisisitiza mwenyekiti huyo.
Kwa
upande wake ofisa mtendaji wa Kijiji cha Sambaru,Baraka Njiku licha ya
kukiri kwamba alishiriki kuanzishwa kwa shule hiyo kuanzia mwanzo mpaka
sasa na walipokutana na uongozi wa kata na kujiridhisha kukamilika kwa
taratibu zinazotakiwa kusajiliwa ndipo walipowaita wakaguzi kwenda
kukugua vyumba vya madarasa na nyumba ya mwalimu na kukubaliwa kuomba
usajili wa shule hiyo.
“Baada
ya wakaguzi kukagua vyumba vya madarasa matatu, nyumba ya mwalimu
pamoja na matundu ya vyoo baadaye wakasema kwa hatua mliyofikia mnaweza
mkaomba shule isajiliwe,tulifanya hivyo,tulipewa idadi ya wanafunzi
waliopo pale shuleni maagizo ambayo aliyapeleka ofisi za mkurugenzi
mtendaji wa wilaya ya Ikungi”aliweka bayana mtendaji huyo.
Hata
hivyo Njiku hakusita kuwatahadharisha viongozi wa chama na serikali
kuacha kuweka kipaumbele masuala ya itikadi za kisiasa kwenye masuala ya
maendeleo ili shule hiyo iweze kufanikiwa kupatiwa usajili kwani
mwakani wanafunzi hao haifahamiki watafanya mtihani wa kuingia darasa la
sita katika shule gani.
Naye
mwenyekiti wa shule ya msingi Sambaru,Senge Jumanne alisema katika moja
ya vikao vyao walivyokutana na mratibu wa elimu kata ya Sambaru
walielezwa masharti ya kusajili shule hiyo kuwa na vyumba vitatu vya
madarasa,nyumba za walimu pamoja na matundu ya vyoo,masharti ambayo
tayari yamekamilishwa na wananchi wa Kitongoji hicho.
Alipotakiwa
kuzungumzia sababu za shule hiyo kutosajiliwa kwa kipindi
kirefu,mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Ikungi,Mohamedi
Nkya licha ya kukiri kutosajiliwa kwa shule hiyo,lakini alisema
amemwagiza ofisa elimu wa wilaya hiyo kulishughulikia suala hilo haraka
iwezekanavyo kabla ya mwezi jan,mwaka ujao ili shule hiyo iwe
imesajiliwa kupunguza usumbufu kwa wanfunzi kutembea umbali mrefu
kufuata elimu.
No comments:
Post a Comment