Siku moja baada ya Dk John Magufuli kupachika jina lake kwenye operesheni ya Chadema ya M4C, Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye amemuelezea mgombea huyo urais wa CCM kuwa ni mtu anayedandia hoja baada ya kupoteza dira.
Wakati
akipewa majibu hayo, DK Magufuli alikuwa akiendelea na kampeni mkoani
Kigoma, ambako ajenda yake kuu ilikuwa ujenzi wa barabara, huku mgombea
wa Ukawa, Edward Lowassa akichanja mbuga mkoani Shinyanga.
Akiwa mkoani Kigoma jana, Dk Magufuli aliwaambia wananchi kuwa kirefu cha nembo ya M4C ni Magufuli for Change, badala ya Movement For Change, ambayo imekuwa ikitumiwa na Chadema kwa miaka takriban sita sasa, ikimaanisha “vuguvugu la mabadiliko”.
Dk Magufuli alisema yeye ndiyo mtu sahihi wa kuongoza mabadiliko na hivyo alama hiyo inatakiwa iwe na jina lake.
Lakini
jana, Sumaye, ambaye ameingia Ukawa bila ya kujihusisha na chama
chochote kati ya vinne vinavyounda umoja huo, jana alisema kauli hiyo ya
Magufuli inaonyesha jinsi yeye na chama chake wanavyotapatapa.
“Ni aibu kubwa,” alisema Sumaye ambaye amekuwa mzungumzaji mkuu kwenye mikutano ya kampeni ya Lowassa.
“Yaani
ni kama mtu anayezama baharini halafu maji yameanza kumuingia puani na
kushindwa kupumua. CCM inazama na sasa inaanza kushika kila mahali kama
mtu anayezama katika maji.”
Sumaye
alisema hayo jana kabla ya Lowassa kupanda jukwaani kwenye mkutano wa
hadhara uliofanyika Uwanja wa Malambo wilayani Bariadi mkoani Simiyu.
Akimchambua
mgombea urais wa CCM, Sumaye alisema kauli yake imeonyesha jinsi
asivyokuwa na aibu na imedhihirisha jinsi alivyopoteza dira kwa kudandia
hoja na mipango ya wapinzani.
“Sisi tunadai mabadiliko na kama na dawa ya kunguni ni kukitoa kitanda na kukitupa nje wakaozee huko,” alisema Sumaye huku akishangiliwa na wananchi.
Kwenye
mkutano huo, Lowassa aliyepokewa na maelfu ya wananchi waliokuwa
wakimsubiri, aliahidi kumaliza kero ya maji kwenye wilaya kwa kuendeleza
mradi wa kutumia maji ya Ziwa Victoria lililopo umbali wa kilomita 30.
Mbunge
huyo wa zamani wa Monduli alifika eneo hilo saa 10:00 jioni na
kukimbiliwa na wananchi waliotaka kumshika na kusababisha polisi kutumia
nguvu ya ziada kuwazuia.
Akizungumza
na wananchi wa Bariadi, Lowassa alirudia tena ahadi yake ya elimu ya
bure akisema kuanzia Januari mwakani hakuna mwanafunzi atakayelipa ada
kuanzia darasa la kwanza hadi chuo kikuu.
Pia
aliahidi kuboresha kilimo ili kiwe cha kisasa na cha kibiashara, huku
akisisitiza msimamo wake kuwa Serikali yake haitamvumilia mtu
atakayeshindwa kwenda na kasi yake.
Mgombea huyo pia alifanya mikutano mingine Maswa na Busega.
No comments:
Post a Comment