19 Sept 2015

Serikali Kushusha Bei ya Umeme Ifikapo Oktoba Mwaka Huu


Serikali imesema bei ya umeme nchini inatarajiwa kushuka kwa kiwango kikubwa baada ya kuanza uzalishaji wa nishati hiyo kwa kutumia gesi asilia kutoka Mtwara hadi Kinyerezi, Dar es Salaam.

Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene alisema hayo, Dar es Salaam, jana wakati akikagua mradi wa bomba la gesi na kuwashwa kwa mitambo ya kuzalisha umeme ya Ubungo II na Kinyerezi I.

Simbachawene alisema bei ya nishati hiyo itakuwa chini ili Watanzania wapate umeme wa uhakika.

“Jambo hili ni kubwa na la kihistoria kwa nchi hii kwa kitendo cha kuanza kutumia umeme wa gesi, tulipaswa kusimama hata kwa dakika tatu kusherehekea mafanikio haya kupitia mradi kubwa wa serikali uliogharimu dola za Marekani 1.22 bilioni,” alisema Simbachawene.

Alisema mitambo ambayo itawashwa kwa kutumia umeme wa gesi ni Ubungo II, Kinyerezi I na Tegeta ambayo kwa ujumla ndiyo itasaidia kutatua tatizo la mgao wa umeme kwa sababu awali ilikuwa haifanyi kazi kwa kukosa gesi.

“Kwa kiasi kikubwa mradi huu wa kufua umeme kwa gesi umekamilika nchini na ndani ya mwezi Septemba na Oktoba, mwaka huu, mitambo yote yenye uwezo wa kuzalisha megawati 335 itakuwa imewashwa na hivyo kuondoa tatizo la umeme hapa nchini, ”alisema Simbachawene na kuongeza:

“Juzi (Septemba 17) tuliwasha umeme wa jumla ya megawati 90 kutoka katika mitambo ya Tanesco ya kuzalisha umeme wa gesi ya Symbion na Ubungo II yenye urefu wa futi za ujazo wa bomba 20milioni na zoezi hili linaendelea hadi Oktoba 20, mwaka huu”.


Simbachawene alisema hilo litakuwa limekamilika kwa kuzalisha megawati 335 na nchi kuingia katika uchumi wa kati.

No comments:

Post a Comment