Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.
-Yafaulu mtihani wa kupata bilioni 992.8 za kuboresha sekta ya umeme
-Yafanikiwa baada ya kutimiza masharti yote likiwemo la kupambana na rushwa
-Zitaanza kutolewa mwakani baada ya kupigiwa kura na Bodi ya MCC
Tanzania imetimiza masharti yote ya kupatiwa raundi ya pili ya fedha za maendeleo kutoka Shirika la Maendeleo ya Milenia la Millennium Challenge Corporation (MCC) la
Marekani na itaanza kupata na kunufaika na mabilioni hayo ya fedha
baada ya wajumbe wa Bodi ya MCC kupiga kura ya kuidhinisha kutolewa kwa
fedha hizo chini ya Mpango wa MCC-2.
Habari hizo
njema zimetangazwa Jumamosi, Septemba 26, 2015, kwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, na Mtendaji Mkuu
wa MCC, Bi. Dana J. Hyde katika mkutano uliofanyika katika Hoteli ya JW
Marriot Essex House, New York, na kuhudhuriwa na watumishi waandamizi
wa MCC akiwamo Bwana Kamran Khan, Makamu wa Rais wa Operesheni za MCC.
Rais Kikwete yuko New York kuhudhuria shughuli za mwaka huu za Baraza
Kuu la Umoja wa Mataifa.
“Hongera
Mheshimiwa Rais kwa sababu nchi yako, Tanzania imetimiza masharti yote
ya kupata fedha nyingine chini ya mpango wa MCC – 2, ikiwa ni pamoja na
uongozi wa MCC kuridhika kuwa Tanzania inachukua hatua za dhati
kupambana na rushwa,” Bi. Hyde amemwambia Rais Kikwete na
viongozi wengine wa Tanzania akiwamo Waziri wa Nchi za Fedha wa
Zanzibar, Mheshimiwa Yusuf Omar Mzee.
Bi. Hyde
amemwambia Rais Kikwete kuwa Bodi ya MCC, katika mkutano wake wa
Septemba 17, mwaka huu na chini ya Mwenyekiti wake, Waziri wa Mambo ya
Nje wa Marekani, Bwana John Kerry, imeafiki kuhusu kipengele pekee
kilichokuwa kimebakia katika masharti ya kupata fedha za MMC kuwa ni
kweli Tanzania inakabiliana ipasavyo na rushwa na kuchukua hatua stahiki
kukabiliana na janga hilo la rushwa.
MCC imetoa
taarifa ya kuthibitisha kuwa Tanzania imetimiza masharti ya kuiwezesha
kufaulu kupata raundi ya pili ya fedha za maendeleo na pia imetoa
taarifa ya kuthibitisha kuwa ni kweli Bodi ya MCC imeridhishwa na hatua
zinazochukuliwa kukabiliana na rushwa.
Tofauti na
fedha nyingi zinazotolewa na wafadhili wengi duniani, fedha za MCC
hazitakiwi kurudishwa na nchi inayopewa fedha hizo na pia nchi husika
hupewa uhuru wa kuchagua aina ya miradi ya maendeleo ambayo inaitaka
igharimiwe na fedha hizo.
Miongoni
mwa wajumbe wengine wa Bodi ya MCC ni pamoja na Waziri wa Fedha wa
Marekani ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi, Mwakilishi wa Biashara wa
Marekani duniani, Mwendeshaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa
la Marekani (USAID), nafasi ambayo kwa sasa anaikaimu Bwana Alfonsi
Lenhardt, Mtendaji Mkuu wa MCC Bi. Hyde na Rais wa Taasisi ya
International Republican Institute (IRI) Balozi Mark Green.
Mabalozi
Lenhardt na Green walikuwa mabalozi wa Marekani katika Tanzania wakati
wa majadiliano, upitishaji na utekelezaji wa MCC–1.
Bi Hyde
amesema sasa linalobakia ni kwa wajumbe wa Bodi kupelekewa muhtasari wa
kuidhinisha mabilioni hayo kwa Tanzania ambayo chini ya mpango wa
uwekezaji wa MCC–2 yatakwenda katika kuboresha huduma za umeme katika
Tanzania ikiwa ni pamoja na kusambaza umeme katika vijiji vingi zaidi
nchini. Kiasi cha asilimia 46 ya Watanzania kwa sasa wanapata umeme
kutoka asilimia 10 ya mwaka 2005 na sehemu kubwa ya asilimia hiyo
imetokana na msaada wa MCC-1.
Chini ya
Mpango huo wa pili wa MCC, Tanzania itapatiwa kiasi cha dola za Marekani
milioni 472.8 (sawa na sh. bilioni 992.80). Kwa kutilia maanani kiasi
cha dola milioni 698 (sawa na sh. trilioni 1.46) ambazo zilitolewa chini
ya MCC-1 basi Tanzania itakuwa imepata jumla ya dola za Marekani
trilioni 2.45 za maendeleo kutoka Marekani katika kipindi cha miaka 10
tu iliyopita. Fedha za MCC-2 zitaanza kutolewa mwakani, 2016.
Kiasi
kilichotolewa kwa Tanzania wakati wa MCC-1 ndicho kilikuwa kiasi kikubwa
zaidi ambacho kimepata kutolewa na Marekani chini ya Mpango huo wa
Millennium Challenge Corporation na kwa kupita MCC-2 Tanzania itakuwa ni
nchi ambayo itakuwa imepata kiasi kubwa cha fedha za maendeleo chini ya
MCC duniani.
Fedha zilizotolewa chini ya MCC -1 zilitumika kujenga Barabara za Tunduma-Sumbawanga, Tanga-Horohoro na Namtumbo-Songea-Mbinga.
Aidha,
fedha hizo zilitumika kujenga upya mfumo wa huduma za maji kwa ajili ya
miji ya Dar es Salaam na Morogoro na zilitumika kusambaza umeme katika
vijiji vya mikoa 10 ya Tanzania Bara.
Fedha hizo
vile vile zilitumika kutandaza njia ya pili ya kusafirisha umeme chini
ya Bahari ya Hindi kati ya Bara na Tanzania Visiwani na pia zilitumika
kujenga barabara zote kuu za Kisiwa cha Pemba na baadhi ya barabara za
Unguja kwa kiwango cha lami.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.