MGOMBEA ubunge Jimbo la Mbeya Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, amejikuta katika wakati mgumu baada ya msafara wake kushambuliwa na mawe na watu wanaodhaniwa kuwa ni wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika
vurugu hizo, watu wawili wamejeruhiwa akiwamo dereva aliyekuwa
akimwendesha mgombea huyo aliyejulikana kwa jina moja la Gabi, maarufu
kwa jina la DJ BBG, ambao wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya.
Vurugu hizo pia zilisababisha gari aliyokuwa amepanda mgombea huyo kupasuliwa kioo cha mbele.
Vurugu
hizo zilisababisha mgombea huyo ahairishe kuwahutubia wakazi wa Kata ya
Iziwa jijini Mbeya kwa muda, kutokana na kulazimika kuripoti kituo cha
polisi kwa ajili ya kutoa maelezo.
Tukio
hilo la kushambuliwa kwa msafara huo, limetokea saa 11 za jioni katika
Kata ya Ghana – njia kuu ya kuelekea Kata ya Iziwa ambako mgombea huyo
alikuwa anakwenda kuomba kura kwa wananchi.
Wakati
msafara huo ukiwa katika mwendo, ulifika katika eneo la Kata ya Ghana,
ambako kulikuwa na mkutano wa CCM wa kumnadi mgombea udiwani, ndipo
ghafla ulianza kushambuliwa kwa kurushiwa mawe.
“Wakati
wafuasi wa CCM wakiwa kwenye mkutano wa hadhara wa kumnadi mgombea wao
ngazi ya udiwani katika Kata ya Ghana, msafara wa sugu ulipita katikati
ya mkutano huo, hivyo kushindwa kuvumilia na kuanza kurusha mawe huku
wengine wakishikana kutaka kupigana,” alisema mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo.
Wakati
mshikemshike huo ukiendelea, imeelezwa kuwa Sugu alitoa taarifa polisi
kuomba msaada ambapo askari walifika katika eneo la tukio na kufanikiwa
kutuliza vurugu hizo.
Baada
ya polisi kuingilia kati, Sugu alikwenda kituoni na kuchukuliwa maelezo
na baada ya hapo aliruhusiwa kuendelea na shughuli zake, lakini gari
yake T 161 CPP Toyota Land Cruiser VX aliyokuwa akiitumia katika kampeni
zake ilibaki polisi.
No comments:
Post a Comment