18 Sept 2015

Mabalozi wa CCM Wakamatwa Wakiandikisha Namba za Kadi za Wapiga Kura na Kuchana Mabango ya Lowassa Mwanza


POLISI mkoani Mwanza linawashikilia watu watatu kwa makosa mawili tofauti ikiwamo ya kukutwa wakiandikisha namba za kadi za wapiga kura na kuchana mabango ya mgombea Urais wa Chadema, Edward Lowassa.

Watuhumiwa hao ambao baadhi yao ni mabalozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) walikamatwa jana na wananchi kwa nyakati tofauti katika eneo la Mtaa wa Utemini na stendi ya Nyegezi jijini mwanza.

Mabalozi wa CCM waliokamatwa wakiandikisha namba za kadi za wapiga kura ni Charles Bukindu wa shina namba 11 na Sola Chule, aliyekamatwa akichana mabango ni Lazaro Nyaruga ambaye anasimamia choo cha stendi ya mabasi Nyegezi.

Inaelezwa watuhumiwa hao waliokamatwa na wananchi na kufikishwa katika kituo cha Polisi Igogo, wanadaiwa kuchukua namba za kadi za mpiga kura kwa maagizo ya viongozi wa juu wa CCM ambao hawajabainishwa majina yao.

Mkuu wa kituo cha Polisi Igogo, Samwel Kilabuko, amekiri watuhumiwa hao kushikiliwa na amesema wameanza uchunguzi, na taarifa kamili itatolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Utemini, Jukael Misigiri, amesema tangu juzi alianza alipata taarifa kutoka kwa wananchi kwamba kuna mabalozi wanapita nyumba hadi nyumba wakiandikisha majina na namba za kadi za wapiga kura na kuanza kuwasaka watuhumiwa hao.

Misigiri amesema baada ya taarifa hiyo kwa kushirikiana na baadhi ya wananchi walianza ufuatiliaji na kufanikiwa kuwafahamu watu hao kuwa ni mabalozi wa CCM ambao aliamua kuwaita ofisini kwake na walipohojiwa walikiri kufanya kazi hiyo.

“Nilipo wahoji kwa nini wanaandika namba za kadi za mpiga kura, walisema wameagizwa na viongozi wa juu wa CCM na wakasema agizo hilo ni la nchi nzima, walianza kufanya kazi hiyo tangu Septemba 16 Mwaka huu,” amesema Misigiri.

Misigiri amesema mpaka sasa baadhi ya watu waliochukuliwa namba za kadi zao na kutoa malalamiko ni wanne, ambao ni Abel Mpabanayo, Veroni Temba, Maliam Paulo na Abel Enock na kwamba kuna wengine zaidi ya 80 walioandikishwa wanaogopa kujitokeza.

Katibu Mwenezi wa Chadema wilaya ya Nyamagana, Andrew Kanichi amesema kitendo cha mabalozi wa CCM kuanza kazi ya kuandika namba za vitambulisho kutasababisha nchi kuingia kwenye machafuko.

Amesema kufuatia hatua hiyo Mkurugenzi wa jiji la Mwanza, Hassan Hida, ambaye ndiye msimamizi wa uchaguzi, anapaswa kuchukua hatua haraka ili kusimamia makubaliano waliyokubaliana na viongozi wa vyama vyote.

Kanichi amesema endapo msimamizi huyo atashindwa kuchukua hatua hiyo kama viongozi wa vyama wanao uwezo wa kusimamia na kuwachukulia hatua stahiki watu wanafanya vitendo hivyo kinyume na makubaliano.

Kuhusu Mabango
Akizungumza nje ya kituo hicho cha Polisi, mmoja wa wananchi waliomkamata mtuhumiwa wa uchanaji wa mabango ya mgombea Urais wa Chadema, Edward Lowassa, Rashid Ramadhan amesema walimuona mtuhumiwa huyo akichana bango la kwanza kwa madai hataki kuona picha ya mgombea huyo.

Ramadhan amesema baada ya kuona kitendo hicho walianza kumhoji sababu za kuchana mabango na alipobanwa zaidi alikimbia na alipokimbia walimkimbiza na kumkamata na kumfikisha katika kituo cha Polisi Igogo.

Amesema licha ya kuwepo kwa mabango mengine ya wagombea wa vyama vingine ikiwemo la mgombea Urais wa CCM, Dk. John Magufuli, hakuyaguswa kitendo ambacho kiliwaumiza na kumkamata ili kutoa fundisho kwa watu wengine.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo, amekiri kutokea kwa matukio hayo mawili na kwamba mpaka sasa wanaendelea na uchunguzi ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.

No comments:

Post a Comment