15 Sept 2015

Maalim Seif aahidi kupandisha bei ya zao la mwani pindipo akichaguliwa kuwa Rais





Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia CUF, Maalim Seif Sharif Hamad akiwahutubia wananchi wa Tumbe alipotembelea eneo hilo.


Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amewaahidi wakulima wa zao la mwani Zanzibar kuwa atapandisha bei ya zao hilo mara moja, iwap atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu wa mwezi ujao.

Maalim Seif alisema bei wanayolipwa wakulima ya shilingi 700 na 800 hivi sasa ni ndogo na hailingani na gharama wanazozitumia wala haiwasaidii wakulima wengi wao wakiwa ni akinamama katika kuondokana na umasikini.

Mgombea huyo ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar alisema hayo alipowatembelea wakulima wa mwani, wakulima wa mpunga na kukagua soko la mboga mboga na samaki katika majimbo ya Tumbe na Konde, mkoa wa Kaskazini Pemba.

Awali katika risala ya wakulima wa mwani na wavuvi wa maeneo hayo iliyosomwa na Aisha mour Ali walisema wanakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa vifaa, bei isiyoridhisha na kukosa boti za kisasa za kufanyia shughuli za uvuvi.

“Tangu 1994 tulipoanza kulima mwani hatujafaidika na bei tunayo lipya, shilingi 700 tunazopewa hazilingani na ugumu wa kazi hii na hilo tumelilalamikia miaka mingi”, walisema katika risala hiyo.

Maalim Seif alisema utafiti uliofanywa unaonesha iwapo wakulima wa mwani watawezeshwa kutumia mbegu za kisasa na kufanya kazi kitaalamu zaidi, zao hilo linaweza kutoa mchango mkubwa katika juhudi za kuwatoa wakulima katika umasikini.

Aliaahidi kuwa akichaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar atahakikisha wanaleta wataalamu wa kutosha kutoa mafunzo ya uzalishaji bora wa zao hilo, kutafuta vifaa pamoja na mbinu mbadala kuliongezea thamani za la mwani.

“Azma yangu ni kuona wakulima wa mwani wananufaika na jasho lao kama vile wanavyonufaika wakulima wenzao wa zao la karafuu”alisema Maalim Seif.

Aidha, aliahidi kuwa atahakikisha mwani unaozalishwa Zanzibar una sarifiwa (processing) kabla a kuuzwa na kuondokana na utaratibu wa kuuzwa mzima, utaratibu ambao huukosesha thamani kubwa katika soko la Kimataifa.

Kilimo cha zao la mwanai kimepata umaarufu mkubwa Zanzibar kwa kujumisha wakulima katika vijiji vya mwambao wa bahari, wengi wao wakiwa ni akina mama, kwa mwaka wastani wa tani 13, 000 huzalishwa Zanzibar na kuuzwa nje ya nchi.

Kuhusu uvuvi, Malim Seif alisema azma yake ya siku nyingi ni kuhakikisha wavuvi kote Zanzibar wanapatiwa vyombo vya kisasa vya uvuvi ambavyo vitawawezesha kufanya shughuli zao kwa ufanisi mkubwa.

Alieleza kuwa kinachojitokeza hivi sasa ni kupungua kwa samaki katika eneo la mwambao wa visiwa, hivyo atahakikisha anaandaa mikakati ya kuwawezesha wavuvi wa Zanzibar ambao wanafikia 32, 000 kufanya shughuli hizo katika bahari ya kina kirefu ambapo kuna samaki wa kutosha.

Sambamba na mikakati hiyo, Maalim Seif alisema atafanya kila njia kuhakikisha zao la mpunga linazalishwa kisasa chini ya utaratibu wa umwagiliaji maji, kwa vile mchele ndio chakula kikuu kwa watu wa Zanzibar.

Akizungumza na wakulima wa mpunga katika mabonde la kinyakuzi na Saninga alisema nia yake ni kuhakikisha Zanzibar inapunguza utegemezi wa bidhaa za chakula kutoka nje ya nchi na iweze kuzalisha asilimia 60 ya mahitaji yake ya chakula hasa mchele.

“Mipango hiyo itawezekana bila wasi wasi, nitaanzisha benki maaluma ya kusaidia wakulima, wavuvi na wajasiriamali na wataweas kupata mikopo yenye masharti nafuu”, aliahidi Maalim Seif.


Aliwataka watendaji wa Halmshauri ya Wilaya ya Micheweni kutafuta watu wenye uwezo wa kuliendesha soko jipya la kisasa lililopo katika kijiji cha Tumbe ili liweze kutumika na kuwanufaisha wakaazi wa maeneo hayo.

No comments:

Post a Comment