16 Sept 2015

JK Kueleza Umoja wa Mataifa Maendeleo ya Kazi ya Jopo Analiliongoza.

Mwenyekiti wa Jopo  la Ngazi ya  Juu kuhusu Mwitikio wa Kimataifa wa Majanga ya Kiafya, Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete anatarajiwa Ijumaa wiki hii  kuwasilisha mbele ya  wajumbe wa nchi wanachama wa Umoja  wa Mataifa  maendeleo ya kazi ya  Jopo   tangu lilipoundwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki  Moon,  mwezi  April  mwaka huu.  

Na  MwandishiMaalum, New York
Rais Jakaya Mrisho Kikwete,  ambaye ni Mwenyekiti wa Jopo la Ngazi ya Juu kuhusu Mwitikio wa Kimataifa wa Majanga ya Kiafya, anatarajiwa Ijumaa wiki hii, kuelezea mbele ya wajumbe wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhusu maendeleo ya kazi ya jopo hilo tangu kuundwa kwake.

Jopo la Ngazi ya juu kuhusu mwitiko wa Kimataifa wa majanga ya kiafya liliundwa mwezi wa nne mwaka huu na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,  Ban Ki  Moon, ambapo Rais Kikwete amepewa jukumu la kuongoza jopo hilo.

Taarifa ambazo zimeufikia Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, zimebainisha kuwa Mhe. Rais atawazungumza na wajumbe wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa tatu wa jopo hilo unaofanyika hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.

Wajumbe wengine wa Jopo hili ni Bw. Celso Amorim( Brazil), Micheline Calmy ( Switzerland), Marty Natalegawa  ( Indonesia) Joy Phumapi ( Botswana) na Rajav Shah ( USA).

Jukumu kubwa ya jopo hilo kwa mujibu wa hadidu rejea,pamoja na mambo mengine,ni kutoa mapendekezo ya namna ya kuimarisha mifumo ya kitaifa na kimataifa katika kuzuia na kukabiliana na majanga ya kiafya ikiwa ni pamoja na kujifunza kuhusu mwitikio wa Jumuiya ya Kimataifa kufuatia kuibuka kwa janga la ugonjwa wa Ebola.

Katika utekelezaji wa majukumu yake Jopo limekuwa likikutana na kufanya majadiliano ya kina na makundi mbalimbali ya kiwamo ya wataalamu, wawakilishi wa nchi tatu ambazo zimeathirika sana na ugonjwa wa ebola (  Liberia,  Siera Leonena Guinea),Mashirika ya Kimataifa na Kikanda , Taasisi za Fedha za kimataifa, wahudumu wa Afya, Wasomi ,Watafiti,  Sekta Binafsi na wataalam wa fani na kada mbalimbali.

Pamoja na kuhudhuria na kuongoza mikutano ya Jopo, Mhe,  Rais Kikwete akiwa hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, pia atahudhuria Mikutano Mikubwa miwili ambayo ni, Mkutano wa Kilele wa Kisiasa, ambao Wakuu wa Nchi na Serikali watapitisha Malengo ya Maendeleo Endelevu ( SDGs). Mhe. Rais atazungumza katika mkutano huu muhimu kwa mstakabali wa maendeleo na ustawi wa binadamu kwa miaka 15 ijayo.

Malengo Mapya ya Maendeleo ya nachukua nafasi ya Malengo ya Maendeleo ya Millenia( MDGs) yanayomaliza muda wake mwishoni mwa mwaka.

Aidha Mhe. Rais atashiriki na kuhudhuria Mkutano wa  70 wa Baraza Kuu la   Umoja wa Mataifa.

Na anarajiwa kuzungumza na Baraza Kuu na hii itakuwa ni hotuba yake ya mwisho akiwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Vile vileMhe. Rais atahudhuria mikutano mingine kadhaa. Baadhi ya mikutano hiyo ni ule ambao umeandaliwa kwa pamoja baina ya Kansela wa Ujerumani Mhe. Angela Merkel ,  Waziri Mkuu wa  Norway   Mhe. Erna Solberg na Rais wa Ghana Mhe.   John Dramani Mahama.

Mhe Rais anahudhuria mkutano huu kwa mwaliko rasmin aliopewa na Kansela Angela Markel. 
Washiriki na waandaji wengine wa mkutano huu ni Mfukowa Bill na Melinda Gates, Shirika la  Afya Dunia (WHO) na Bank ya Dunia.


Mkutano huu unatarajiwa kuzindua misingi na hatua muhimu ambazo zinataratibu ufanisi na upimaji wa matokeo ya juhudi za kuimarisha mifumo ya afya.

No comments:

Post a Comment