22 Sept 2015

Emmanuel Mbasha Aachiwa Huru...Upande wa Mashtaka Umeshindwa Kuthibitisha kosa la Ubakaji dhidi yake



Mwimbaji wa nyimbo za Injili nchini, Emmanual Mbasha (32), leo ameangua kilio baada ya kuachiwa huru na Mahakama ya Wilaya ya Ilala huku mke wake, Flora amesema yuko tayari warudiane endapo ataomba radhi.

Mbasha alimwaga chozi muda mfupi baada ya kutoka katika chumba cha Mahakama alipopandishwa kizimbani kusomewa hukumu.

Mshtakiwa huyo ameachiwa huru dhidi ya kesi ya ubakaji iliyokuwa ikimkabili baada ya upande wa mashtaka kushindwa kudhibitisha kosa.

Mwimbaji huo ambaye kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo alionekana hana furaha, alifikia uamuzi huo wa kulia mara tu baada ya kusomwa kwa hukumu hiyo, ambapo alipotoka nje ya chumba cha mahakama alipiga magoti chini huku akiinua mikono juu na kulia kwa sauti huku akisema ‘mungu ni mwema’.

Mbasha anakabiliwa na mashtaka mawili ya kumbaka shemeji yake mwenye umri wa miaka 17 huku akijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria

Kesi hiyo namba 186 ya mwaka 2014, imeendeshwa kwa mwaka mmoja na miezi miwili na kwa mara ya kwanza alifikishwa mahakamani hapo Juni 17 mwaka 2014.

Akisoma hukumu hiyo leo, hakimu Mkazi Flora Mujaya alisema mahakama imemuachia huru baada ya upande wa mashtaka kushindwa kudhibitisha kosa lililokuwa likimkabili.

“Mahakama yangu imemuachia huru Mbasha baada ya upande wa mashtaka kushindwa kudhibitisha kosa ”alisema Hakimu Mujaya.

Hakimu Mujaya alisema mahakama hiyo imetoa uamuzi huo baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi sita wa upande wa mashtaka vikiwemo vielelezo vilivyotolewa mahakamani hapo kama ushahidi.

Hukumu hiyo, ilipaswa kutolewa wiki iliyopita , lakini iliahirishwa hadi leo kwa sababu hakimu huyo ambaye ametoa hukumu hiyo leo alikuwa likizo .

Mke wa Mbasha, Flora alisema yeye na familia yake wanaheshimu maamuzi yaliyotolewa na Mahakama dhidi ya Mbasha na kwamba anaiomba familia yake ikubaliane na maamuzi hayo na suala la kukata rufaa lisiwepo.

“Mimi na familia yangu tunaheshimu uamuzi wa mahakama na ninaiomba familia yangu ikubaliane na uamuzi huu uliotolewa na mahakama na suala la kukata rufaa lisiwepo kwani uamuzi wa mwisho upo katika familia” alisema Frola alipotafutwa kwa simu.