MGOMBEA
urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli pamoja na
mwenzake kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), chini ya
mwamvuli wa Ukawa, Edward Lowassa, jana walifika mahakama kuu kanda ya
Dar es Salaam kwa ajili ya kusaka viapo vya mahakama kuthibitisha
rasmi kuwania nafasi hiyo.
Magufuli
na Lowassa kwa sasa wamekuwa mahasimu wa kisiasa tangu waziri mkuu huyo
wa zamani alipotangaza kuihama CCM baada ya mchakato wa urais
uliofanyika mjini Dodoma Julai mwaka huu.
Wagombea
hao walikwenda jana Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na kupewa fomu
kila mmoja kwa wakati wake ya kumthibitisha kuwania nafasi hiyo ya juu
katika uongozi wa nchi.
Wagombea
hao walithibitisha fomu hizo mbele ya Jaji Sakieli Kihiyo kwa matakwa
ya kanuni za uchaguzi wa Rais na Bunge za mwaka 2015.
Magufuli na Samia
Dk.
Magufuli alikwenda mahakamani hapo akiwa ameandamana na mgombea mwenza
wake, Samia Suluhu Hassan mbele ya Jaji Kihiyo saa tano na walikaa
katika chumba cha mahakama kwa zaidi ya saa moja kwa ajili ya kusaini.
Baada ya kumaliza kuapa na kusaini Dk. Magufuli alitoka nje ya mahakama na kuzungumza kwa kifupi na wanahabari.
“Katika
fomu ya kugombea nafasi ya urais inaeleza kwamba mtu anayetaka kushika
madaraka makubwa azingatie kanuni na sheria zilizoainishwa .
“Kilichonileta
hapa leo (jana) ni kukamilisha sehemu ya kanuni na sheria, kukagua fomu
kwa ukamilifu na kusaini kiapo, naomba Watanzania waniombee,”alisema na kuondoka.
Lowassa atua
Waziri
Mkuu Mstaafu, Lowasa alifika eneo la mahakama saa saba adhuhuri na
kuelekea moja kwa moja katika chumba cha mahakama kwa ajili ya kuapa na
kusaini fomu ya kugombea urais.
Lowassa
alichukua nusu saa kumaliza mchakato huo na kutoka na alipotakiwa
kuzungumza na waandishi wa habari alisema hawezi kusema chochote.
“Siwezi kusema lolote, tusubiri Tume ya Uchaguzi ikinipitisha nitazungumza,”alisema kwa kifupi Lowassa.
Msajili Mahakama Kuu
Akitoa
ufafanuzi kwa waandishi wa habari Msajili wa Mahakama Kuu John Kahyoza,
alisema katika fomu za kugombea udiwani, ubunge na urais kuna kipengele
cha tamko au kiapo cha kisheria cha mgombea.
“Leo
wagombea urais wamekuja kuthibitisha kwa kiapo waliyoyajaza katika fomu
ya kugombea nafasi hiyo ni sahihi, wamefanya hivyo kwa matakwa ya
kanuni za uchaguzi na Bunge za mwaka 2015.
“Miongoni
mwa wanayothibitisha ni kwamba wao ni raia wa Tanzania, wametimiza umri
unaohitajika kisheria, hawajawahi kutiwa hatiani na kufungwa kwa kosa
lolote ikiwemo kukwepa kodi.
“Fomu
ikisharudishwa na kubainika kwamba miongoni mwa waliyoapa walisema
uongo ni kosa la jinai hivyo aliyeapa anastahili kuchukuliwa hatua,”alisema.
Alisema
madiwani na wabunge wanatakiwa kuapa mbele ya hakimu lakini haikueleza
ni hakimu wa mahakama gani hivyo wanaweza kuapa kwa hakimu wa mahakama
yoyote.
Alipoulizwa
sababu ya Dk. Magufuli kutumia zaidi ya nusu saa, Kahyoza alisema
wagombea urais walitakiwa kupita katika mikoa kumi kwa ajili ya kusaka
wadhamini hivyo fomu zinatakiwa ziwe 40.
“Kundi la kwanza lililoingia la Dk. Magufuli lilikuwa na fomu zote 40, zikathibitishwa na kusainiwa.
“Kundi
la pili la Lowassa waliingia na fomu zao nne, nikawauliza wakajibu
ndizo walizoelekezwa, nikawashauri wakaongeze mbili, walifanya hivyo
zikathibitishwa na kusainiwa.
“Kwa maana hiyo fomu 34 hazikuingia kwa ajili ya kusainiwa, sisi hata mgombea akija na fomu moja anasainiwa,”alisema na kuongeza kwamba hiyo ndiyo sababu iliyofanya mmoja atumie muda mwingi na mwingine atumie muda mfupi
No comments:
Post a Comment