Urais 2015: Benard Membe Anusurika Kufa Baada ya Ndege yake Kutaka Kugongana "Uso kwa Uso" na Ndege Nyingine - LEKULE

Breaking

12 Jun 2015

Urais 2015: Benard Membe Anusurika Kufa Baada ya Ndege yake Kutaka Kugongana "Uso kwa Uso" na Ndege Nyingine

Mio  za kuwania kumrithi Rais Jakaya Kikwete miongoni mwa makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) zimezidi kushika kasi, safari hii Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, akinusurika kifo baada ya ndege aliyokuwa akisafiria kuwapo katika hatari ya kugongwa na ndege nyingine angani alipokuwa akielekea Zanzibar.
 
Waziri Membe akiwa na ujumbe wake wa watu nane walikuwa wakisafiria ndege ya kukodi kampuni ya 5H NEG Precision Aviation ikirushwa na rubani Mathew Mhahiki ambaye ameonesha kushangazwa na tukio hilo alilodai “ni kwa rehema za Mungu tumepona ajali hii.” 
 
Akizungumza na mwandishi wetu, rubani Mathew Mhahiki alisema, “…lazima kuna tatizo katika control center hata hivyo tayari nimeongea nao na wameniomba samahani na kudai walipitiwa maana kwa hali ilivyokuwa ni kwamba tungegongana wakati wa kutua, nimeshangaa tu kuona ndege hii hapa ndio maana nikaamua kumkwepa mwenzangu nikapanda juu.” 
 
Aidha, Waziri Membe aliyeonekana kushitushwa na hali hiyo alisema, “…nina uzoefu mkubwa wa kusafiri na ndege mahali pengi duniani, hali hii ilikuwa ni ajali na labda sasa tungekuwa dead bodies lakini ninajua Mungu yuko upande wetu katika safari hii ya uhakika, lakini pia izingatiwe nimekuja kufanya kazi ya Mungu.” 
 
“Katika safari hii tutashuhudia mambo mengi sana lakini kwa kuwa kila ninapotaka kuondoka nyumbani ama hotelini mara nyingi nimekuwa nikimtanguliza Mungu maana bila Mungu, hii ilikuwa ni mwisho wa maisha yetu tuliokuwa kwenye ndege hii,” alisema Membe 
 
Naye mwanasiasa anayenyemelea Ubunge Jimbo la Rungwe Mashariki, Richard Kasesela, aliyeongozana na Waziri Membe alionesha wasiwasi wa hali hiyo kuwa inaweza kuwa ni hujuma dhidi ya Membe.
 
“Katika hali ya kawaida watu wa control center hawawezi kuruhusu ndege mbili kutua kwa wakati mmoja maana tafsiri yake ni kuwa mtagongana na ndio maana kuna haja ya kujua ni kwa nini hali hii imetokea katika kipindi hiki cha Waziri Membe na wanasiasa wengine wanapotafuta kuungwa mkono kugombea nafasi ya urais kupitia Chama Cha Mapinduzi,” alisema Kasesela 
 
Taarifa nyingine kuhusu tukio hilo zinabainisha kuwapo kwa uzembe katika chumba cha kuongozea ndege ambapo mmoja wa wafanyakazi katika chumba hicho alithibitisha uzembe huo. 
 
“Mimi si msemaji wa ofisi yetu lakini hata sisi tumeshangazwa na hali hiyo maana si jambo la kawaida kutokea kama hakuna tatizo. Wengine tayari tulishika vichwa maana uzoefu unaonesha kuwa ukiruhusu ndege mbili kutua kwa wakati mmoja ni wazi unataka kusababisha ajali,” alisema kwa sharti la hifadhi ya jina. 
 
Waziri Membe alikuwa amealikwa mjini Zanzibar na Umoja wa Kinamama wa Kikristu (UMAKI) wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Zanzibar, waliokuwa wakifanya mkutano wao mkuu unaofanyika kila baada ya miaka mitano akitokea Iringa ambako alikwenda kutafuta wadhamini ili kumwezesha kugombea urais kupitia CCM. 
 
Akiwa uwanjani hapa Waziri Membe alikutana na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba aliyekuja  Zanzibar kutafuta wadhamini ambapo makada hao walipata nafasi ya kuzungumza na kujadiliana masuala ya siasa ndani ya chama chao. 
 
Akiwa katika mkutano wa kinamama hao, Membe alisema; “Miongoni mwa mambo yanayonikera ndani ya nafsi yangu ni kuona mwanamke bado anaachwa nyuma, hili halipendezi ni lazima tuhakikishe wanawake wanapata elimu ya ufundi stadi maana mwanamke akiwezeshwa hasa katika eneo hili la ujuzi, wanaweza hata kushinda wanaume wengi.” 
 
“Ni lazima kina mama wawezeshwe kujiajiri ili msiwategemee kina baba kwa kila jambo lakini pia ili kufikia malengo hayo ni lazima tuwape elimu kina mama.” 
 
Kina mama hao pamoja na mambo mengine wameonesha miradi mbalimbali wanayoifanya ikiwa ni pamoja na utengenezaji wa bidhaa mbalimbali kama mishumaa, asali iliyosindikwa, vitenge, siagi na bidhaa mbalimbali za nyumbani. 
 
Membe ameahidi kuwasaidia kumpata mfadhili wa kujenga kituo cha umoja huo na hasa jengo la utawala huku akisisitiza umoja huo pamoja na mambo mengine, kujenga kituo cha watoto yatima pamoja na mradi wa maji. 
 
Awali, akiwa mkoani Iringa Membe alisema; “Hebu wapimeni hao wanaokuja kwenu kwa fedha kutaka kuwanunua ili kuwaunga mkono, ni hatari maana kama kiongozi utajisikiaje kumtumikia mtu ambaye tayari ulimnunua kwa fedha” 
 
Aliwataka wananchi kupokea fedha wanazopewa na baadhi ya wanasiasa wanaowania urais lakini akisisitiza wawe na msimamo. 
 
“Hizo ni fedha zenu zichukueni mle lakini muwe na msimamo wa kutomchagua mtu wa namna hiyo maana hatoweza kuwatumikia maana atakuwa na haya,” alisema Membe 
 
Akizungumzia vipaumbele vyake endapo atachaguliwa kuwa mgombea urais na hatimaye Rais wa Tano wa Tanzania, Waziri Membe alisema atahakikisha nchi inapiga hatua za maendeleo kwa haraka kupitia uchumi wa viwanda vinavyotegemea kilimo. 
 
“Badala ya kuuza pamba sasa tuuze nguo, badala ya kuuza ngozi sasa tuuze viatu na kadhalika, uchumi wa namna hii unaweza kutoa ajira kubwa sana na hasa baada ya kugundulika kwa gesi asilia itakayotusaidia kuondokana na tatizo la nishati ya umeme,” alisema 
 

Akiwa Iringa, alikabidhiwa fomu zenye orodha ya majina ya wanaCCM 317 na Katibu wa CCM Wilaya ya Iringa Mjini, Zongo Zongo. 

No comments: