MWENYEKITI
wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, ameieleza
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuwa, hawakufanya
maandamano wala kupata barua ya zuio badala yake alipigwa na polisi.
Prof.
Lipumba aliyasema hayo mahakamani hapo jana wakati yeye na washtakiwa
wengine waliposomewa maelezo ya awali, mbele ya Hakimu Mkazi, Cyprian
Mkeha.
Mawakili
wa Serikali, Tumaini Kweka, Joseph Maugo na Mohamed Salum, walidai kesi
hiyo imekuja mahakamani hapo kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo
ya awali.
Akisoma
maelezo hayo, Salum alidai CUF waliandika barua Januari 22, mwaka huu,
kwenda kwa Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman
Kova kutoa taarifa ya kufanya maandamano kuanzia Ofisi za CUF Wilaya ya
Temeke kwenda Mbagala Zakhiem.
Alidai
mshtakiwa wa kwanza, Prof. Lipumba ndiye aliyepanga kuongoza maandamano
na baadaye kuhutubia kwenye mkutano wa hadhara uliokuwa ufanyike
Viwanja vya Zakhiem.
Aliongeza
kuwa, Januari 26, mwaka huu, Jeshi la Polisi lilijibu barua hiyo na
kuwataka wasitishe maandamano kutokana na sababu mbalimbali zilizoelezwa
ndani ya barua hiyo.
Baada
ya maelezo hayo, Prof. Lipumba alisema barua hiyo ilifika saa 12:30
jioni hivyo hakupata ujumbe wowote kama wamezuiwa kufanya maandamano
hayo.
Alisema
Januari 27, alifika katika Ofisi ndogo za CUF zilizopo Temeke
kuzungumza na maofisa wa chama hicho na baadaye walianza maandamano
kuelekea Zakhiem.
Hata
hivyo, upande wa Jamhuri ulidai kabla ya maandamano hayo hayajaanza,
polisi walitoa onyo la kuwataka wasitishe maandamano na kutawanyika
kwani wanachokifanya ni kinyume cha sheria.
Licha
ya kutolewa kwa onyo hilo, washtakiwa walikaidi amri hiyo,kuendelea na
maandamano na walipofika eneo la Mtoni Mtongani, walikutana na polisi
ambao walitoa ilani ya kusitishwa kwa maandamano hayo lakini
waliendelea kukaidi.
Baada
ya washtakiwa kukaidi amri ya polisi, waliwakamata, kuwapandisha kwenye
gari na kupelekwa Kituo cha Polisi Kati ili kutoa maelezo.
Hata
hivyo, baada ya kusomewa maelezo na upande wa Jamhuri, mshtakiwa wa
kwanza hadi 29, walikana na kudai hawakukaidi amri hiyo wala kufanya
maandamano.
"Hatukufanya maandamano, huo ni uongo mtupu kwanza sikupata hiyo barua, isipokuwa polisi waliamua kutukamata na kutupiga tu," alidai Prof. Lipumba.
Upande
wa Jamhuri ulidai kuwa, mshtakiwa wa 30 na 31 walikamatwa katika
Viwanja vya Zakhiem wakiwa wamekusanya watu kwa ajili ya kufanya mkutano
shtaka ambalo walilikana.
Kweka aliieleza mahakama kuwa, upelelezi wa kesi hiyo umekamilika, hivyo aliomba ipangwe tarehe ya kusikilizwa.
Baada ya kueleza hayo, upande wa utetezi ukiwakilishwa na Wakili Twaha Taslima aliomba apatiwe maelezo ya mlalamikaji.
Hakimu
Mkeha aliahirisha shauri hilo hadi Juni 4, mwaka huu kwa ajili ya kesi
hiyo kuanza kusikilizwa na kuutaka upande wa Jamhuri kuja na mashahidi
wawili.
Hivi
karibuni, viongozi wa CUF na wafuasi wao walifikishwa mahakamani hapo
na kusomewa mashtaka matatu ikidaiwa kosa la kwanza walilitenda Januari
27, mwaka huu, eneo la Temeke ambapo wote kwa pamoja walikula njama ya
kutenda kosa la kufanya mkusanyiko kinyume cha taratibu.
Katika
shtaka la pili, inadaiwa siku hiyo ya tukio, washtakiwa, wakiwa katika
Ofisi ya CUF karibu na Hospitali ya Wilaya ya Temeke bila ya kuwa na
uhalali, walifanya mkusanyiko kwa nia ya kufanya maandamano kwenda
Mbagala Zakhiem.
Shtaka
la tatu, ilidaiwa siku hiyo ya tukio katika eneo la Mtoni Mtongani,
waligoma na kutojali tangazo halali lililotolewa na polisi likiwataka
wasiandamane na kutofanya mkusanyiko usio halali.
Washtakiwa
hao ni Shabani Tano (29), Shabani Abdallah (40), Juma (54), Athuman
Ngumwai (40), Shaweji Mohamed, Hassan Said (37), Mohamed Ibrahim (31),
Allan Ally (53) na Abdina Abdina (47).
Wengine
ni Allawi Msenga (47), Abdi Hatibu (34), Abdallah Ally (32), Said
Mohamed (40), Salim Mwafisi, Salehe Rashid (25), Rehema Kawambwa (47),
Salma Ndewa (42), Athuman Said (39), Dickson Leasson (37) na Nurdin
Msati (37).
No comments:
Post a Comment