Zitto Kabwe Aipasua Ngome Ya CHADEMA Jijini Mwanza......Melfu ya Wananchi Wafurika Viwanja vya Furahisha Kumsikiliza, Juhudi za CHADEMA Kuvuruga Mkutano Zakwama - LEKULE

Breaking

20 Apr 2015

Zitto Kabwe Aipasua Ngome Ya CHADEMA Jijini Mwanza......Melfu ya Wananchi Wafurika Viwanja vya Furahisha Kumsikiliza, Juhudi za CHADEMA Kuvuruga Mkutano Zakwama



Juhudi za Chama cha Demokrasia na Maendeleo kuuvuruga mkutano wa ACT -Wazalendo jana ziligonga mwamba baada ya Maelfu ya wananchi kufurika katika viwanja vya Furahisha kuwasikiliza viongozi wa chama hicho huku ulinzi ukiwa umeimarishwa katika kila kona ya uwanja huo.

Mpekuzi ilishuhudia Difenda tatu za polisi zikifanya doria katika uwanja huo huku polisi wakiwa tayari kwa lolote.

Ulinzi uliimarishwa katika viwanja hivyo kutokana na kauli ya Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Bara, John Mnyika aliyoitoa juzi katika viwanja hivyo ikiwa ni siku moja tu kabla ya mkutano wa ACT-Wazalendo kufanyika.

Akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Furahisha Mwanza juzi ambao ulihudhuriwa na wafuasi wachache wa chama hicho, Mnyika alisema Chadema haiko tayari kuikaribisha ACT-Wazalendo ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutokana na kile alichosema ‘ni adui kwao’.

Katika hotuba yake, huku akinukuu baadhi ya vifungu vya biblia na Quruan, Mnyika aliwataka wafuasi na wapenzi wa CHADEMA kumkabili Zitto Kabwe kwa namna yoyote kwa kuwa ni adui wa chama chao na ujio wake jijini Mwanza ulikuwa na lengo la kukiharibu chama chao..

“Mtume Muhamad (S.A.W) alikuwa anazungumzia unafiki ambao una sura mbili na sifa zake, leo (ACT) wanasema wapo upinzani, wanasema msiunge mkono Ukawa halafu mnawakaribisha?

“Nendeni kila mahali waambieni wananchi adui yetu mkuu ni Zitto. Sikilizeni niwaambie Taifa hili kama ni ufisadi tumeshazungumzia sana kuanzia EPA mpaka Richmond. Dk. Slaa (Willbrod) alipoingia bungeni aliyasema haya kwa sasa si mapya. Adui yetu ni Zitto na hatumtaki Ukawa,” alisema Mnyika.

Zitto Kabwe Ajibu Mapigo
Akihutubia mamia ya wananchi wa Mwanza jana, Zitto alisema kadri siku zinavyosonga wabaya wake wamekuwa wakijionyesha.

Zitto alisema pamoja na hali hiyo, ACT-Wazalendo haiko tayari kuzungumzia siasa za wakati uliopita kwa vile kufanya hivyo si afya njema kwa siasa za upinzani.

Alisema ni vema viongozi wa vyama vya upinzani waachane na ugomvi binafsi na watangulize masilahi ya taifa mbele.

“Mwanzo walipotufukuza walituambia tukatafute vyama vingine hilo likafanyika, tulipopata vyama vya kufanyia siasa wakasema vipo kwa ajili ya kugawa upinzani tukasema tupo tayari kuunganisha nguvu ya pamoja kwa ajili ya kuiondoa CCM…wenzetu pia hili hawalitaki sasa ni wajibu wenu kutambua watu gani hawataki kuiondoa CCM,” alisema Zitto.

Alisema wao (ACT) wana nia ya dhati lakini wenzao wanaweka ugomvi binafsi mbele ya masilahi ya taifa.

“Sisi ACT Wazalendo bado tupo tayari kushirikiana kwa mujibu wa misingi. Shabaha yetu ni moja tu, kubomoa mfumo wa uchumi wa kinyonyaji na ufisadi ili kujenga uchumi shirikishi wa wananchi,” alisema na kuongeza:

“Sikufundishwa kugombana na watu barabarani au kusema ovyo mitaani, kufanya hivi hakuna tofauti na kumsema mke au mume mlioachana…mmoja kwa kukosa busara na kwa kuwa aliachana na yule mke anaamua kwenda vijiweni na kutoa siri za mzazi mwenzie, hili kwetu hapana.

“Tunakuja na jahazi jipya ambalo ndugu zangu wa Mwanza nimekuja kuwakabidhi, kubwa tunataka kulirudisha taifa katika misingi yake ya ujamaa na kujitegemea, tunahitaji ujamaa wa demokrasia,” alisema Zitto.

Alisema tafsiri ya ujamaa haina maana kuwa chama hicho kitataifisha mali za watu, bali kitarekebisha makosa ya ubinafsishaji kwa kurejesha mali zote za taifa zilizouzwa na wanunuzi hawajatekeleza mikataba yao.

Apata Mapokezi ya Kutisha:
Zitto ambaye amefuatana na Mwenyekiti wa chama hicho, Anna Mghwira, waliwasili Mwanza saa 8.00 mchana na kupata mapokezi makubwa yaliyoanzia wilayani Misungwi.

Alipofika katikati ya jiji la Mwanza, Maelfu ya wananchi waliuzia msafara huo na kuanza kulisukuma Gari la Zitto.

Hali hiyo ilisababisha foleni kubwa ambapo trafiki waliingilia kati na kumtaka Zitto Awashe gari kunusuru Foleni.

Safari ya kulekea Viwanja vya Furahisha iliendelea ambapo mapokezi hayo yakiongozwa na vijana waendesha pikipiki (bodaboda) na kikundi cha wanawake yaliusindikiza msafaa huo hadi ulipoingia kwenye uwanja wa Furahisha.

Leo ni zamu ya Musoma:
ACT- Wazalendo leo wanatarajia kufanya mkutano wa hadhara Musoma.

Habari tulizozipata zinadai kuwa baada ya CHADEMA Kuvuruga jijini Mwanza juzi, jana walikuwa Musoma ambapo kauli yao ilikuwa ni ileile ya kuwataka wananchi kutohudhiria mikutano ya Zitto Kabwe.

No comments: