Naibu Waziri wa Afya Dr Kigwangala Azindua Wodi Mpya Ya Wagonjwa Mahututi Muhimbili.....Kasema Serikali ina Mpango wa Kuacha Kupeleka Wagonjwa Nje ya Nchi Kutibiwa - LEKULE

Breaking

4 Mar 2016

Naibu Waziri wa Afya Dr Kigwangala Azindua Wodi Mpya Ya Wagonjwa Mahututi Muhimbili.....Kasema Serikali ina Mpango wa Kuacha Kupeleka Wagonjwa Nje ya Nchi Kutibiwa


Serikali imesema ina mpango wa kusitisha kupeleka wagonjwa nje ya nchi kupatiwa matibabu na kuhakikisha kila kitengo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kinakuwa na chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU).

Serikali imechukua uamuzi huo, wakati taarifa ndani ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii , Jinsia, Wazee na Watoto zikieleza inadaiwa deni la Sh.28.74 bilioni za malimbikizo kutokana na ongezeko la wagonjwa wanaopelekwa nje kwa matibabu.

Akizungumza jana wakati wa kuzindua chumba cha ICU kilichopo jengo la Mwaisela hospitalini hapo, Naibu Waziri wa wizara hiyo, Dk Hamis Kigwangalla alisema lengo la Serikali ni kuanzisha vyumba hivyo kwa kila kitengo ili kupunguza vifo.

Alisema hospitali hiyo ina vitanda 25 vya ICU, lakini lengo ni kuwa na vitanda 150 vya wagonjwa mahututi na wataalamu wa kutosha.

Alisema Serikali ina mpango wa kutoa mafunzo kwa madaktari na wauguzi watakaokuwa wamebobea katika fani ya vyumba hivyo.

Madaktari na wauguzi hao watapata mafunzo kutoka Chuo Kikuu cha Cairo na mengine yatatolewa kupitia Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (Muhas).

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Lawrence Mseru alisema kuzinduliwa kwa ICU hiyo kunaifanya hospitali hiyo kuwa na vyumba vya aina hiyo viwili vyenye vitanda 25, kutoka chumba cha awali kilichokuwa na vitanda vinane.

Alisema uwapo wa vitanda hivyo ni ongezeko la asilimia 200 ikilinganishwa na uwezo wa awali.

“Fedha za ndani zilizotumika kwa ajili ya ukarabati wa chumba hiki ni Sh230 milioni ikiwa ni pamoja na kutafuta ufadhili kutoka taasisi isiyo ya kiserikali ya Ujerumani iliyowekeza vifaatiba vya Sh600 milioni.

‘‘Mfadhili huyu ndiye aliyetununulia vifaa vyenye thamani ya Dola 800,000 za Marekani,” alisema Profesa Mseru. 
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto, Dkt. Hamisi Kigwangalla akisisitiza jambo jana Jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi ya wodi ya ICU ilizopo kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili(MNH)
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hosptitali ya Taifa ya Muhimbili MNH, Profesa Lawrence  Museru (katikati) akitoa maelezo mafupi jana Jijini Dar es Salaam kwa  Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya  Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamisi Kigwangalla (kulia) wakati wa sherehe za uzinduzi wa wodi ya ICU iliyopo kwenye jengo la Mwaisela katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili(MNH)
Rais wa Shirika lisilo la Kiserikali la Madaktari wanaohusika na magonjwa ya ini na tumbo(Gastrenterology) kutoka Munich Ujerumani(kulia) akiteta jambo na  Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya  Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamisi Kigwangalla wakati wa uzinduzi wa ICU Muhimbili.

No comments: