Mkuu Wa Wilaya Akanusha Familia Kuchemsha Mawe Na Pumba Kutokana na Kukithiri Kwa Njaa - LEKULE BLOG

Breaking

Header Ads

Friday, 1 January 2016

Mkuu Wa Wilaya Akanusha Familia Kuchemsha Mawe Na Pumba Kutokana na Kukithiri Kwa NjaaMKUU wa wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, Mohamed Utaly amekanusha taarifa za watu wa wilayani yake kuchemsha mawe kwa ajili ya kukosa chakula kutokana na kukithiri kwa njaa.

Akitoa taarifa ya hali ya njaa kwa Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Maafa kutoka ofisi ya Waziri mkuu, Mbazi Msuya, mkuu huyo wa wilaya alisema kuna vyombo vya habari na mitandao ya kijamii imeripoti kuwa wananchi wa wilaya ya Mpwapwa wanalazimika kupika mawe na pumba kutokana na wilaya hiyo kukumbwa na njaa.

Utaly pamoja na kukiri kuwepo na njaa alisema waandishi wametia chumvi mno.

“Ukweli katika wilaya yangu kuna njaa hasa vijijini, lakini njaa iliyopo haijafika kiasi cha wananchi kula pumba au kuchemsha mawe kwa ajili ya kuwadanganya watoto ili walale… baadhi ya kaya hula mlo mmoja kwa siku lakini si kula pumba na kuchemsha mawe,” alisema Utaly na kuongeza kuwa chakula kipo lakini changamoto ni ukubwa wa bei.

Mmoja wa wananchi wa kijiji cha Chunyu, Edward Kusena ambaye ni mkulima mkubwa wa muhogo kijijini hapo alisema njaa katika kijiji hicho na wilaya nzima imesababishwa na baadhi ya wananchi kuupuzia maagizo ya wataalamu ya kulima mazao yanayo stahimili ukame na yanayokomaa haraka kama muhogo, mtama na uwele kwa wilaya zenye mvua kidogo kama Mpwapwa.

Ofisa kilimo, uvuvi na umwagiliaji wa wilaya ya Mpwapwa, Justina Munisi alisema pamoja na kuwapo kwa njaa tayari kitengo cha maafa kutoka ofisi ya waziri mkuu imetoa mahindi tani 200 ambayo yamegawiwa kwa vijiji 36 kati ya vijiji 68 vilivyoathiriwa na njaa.

Munis alisema njaa hiyo imesababishwa na ukosefu wa mvua kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2014/2015 na wananchi kutokufuata ushauri wa kupanda mazao yanayostahili kupandwa katika kanda za mikoa kame kama wa Dodoma na wilaya zake.

Mbunge wa jimbo la Mpwapwa, George Lubeleje alishukuru serikali kuwapatia chakula cha msaada tani 200 ambazo alisema hazijakidhi kwa wananchi wote, alitumia fursa hiyo kuiomba serikali kuongeza tena tani 200 ili kuweza kufikia lengo na kupunguza ukali wa njaa kwa Mpwapwa.

Kwa upande wake Msuya aliwataka viongozi wa halmashauri hiyo kuacha kuomba chakula cha msaada bali aliwataka kuomba chakula cha njaa na mbegu ili kuweza kuondokana na kuomba chakula cha njaa kila mwaka.

Pia alisema kitengo chake kitaanza kugawa mbegu za muhogo bure kwa wakulima watakaojiandikisha na kutaka kupanda zao hilo ambalo litaweza kuwa mwarobaini wa wilaya hiyo kukumbwa na njaa kila mwaka.
Post a Comment