RAIS mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete amesema katika uongozi wake wa miaka 10, hakuwahi kuagiza mtu asamehewe kontena lake lisilipe kodi na angefanya hivyo, mapato ya Serikali yasingeongezeka kutoka Sh bilioni 177 kwa mwezi mpaka Sh bilioni 900.
Akizungumza
baada ya kuwashitukiza wananchi wa Chalinze katika soko kuu la eneo
hilo kwa kuungana nao kufanya usafi kuitikia agizo la Rais John Magufuli
jana asubuhi, Kikwete alisema katika uongozi wake hakuwahi kuagiza mtu
anayestahili kulipa kodi asilipe kodi.
Alisema
wakati huu ambao amepumzika baada ya kustaafu, amepata nafasi ya kusoma
mitandao na magazeti mbalimbali na kukuta baadhi ya watu, wakimshutumu
na kumtukana yeye na familia yake wakimhusisha na ukwepaji kodi.
“Ni
afadhali wanishambulie mimi ila wamuache Rais Magufuli (John Pombe)
afanye kazi, ni maneno ya walioshindwa wasinilaumu, aliyewashinda ni
Magufuli sasa hawana la kusema. Ni sawa na siasa za maji taka, lakini
watakuwa wanapoteza muda wao na kufanya kazi bure, kwa kuwa mimi
sigombei kitu chochote tena.
“Wanahusisha
mpaka na familia yangu, kama mimi mwenyewe sijawahi kuruhusu mtu hata
mmoja atoe kontena bila kulipia kodi, siamini kama mke wangu (Mama
Salma) au mwanangu Ridhiwani (Mbunge wa Chalinze), wangeweza kufanya
hivyo tu na watu wakawasikiliza.
“Wanachonga
tu, wengine wamesema Kikwete hachomoki, kwani nimechomeka nini?”
Alihoji na kusababisha watu walioshirikiana naye kufanya usafi katika
soko hilo kucheka na kuanza kushangilia.
Alisema
nafasi ya urais aliyoaminiwa na Watanzania kwa miaka 10, ilikuwa yake
na haikuwa na ubia na mkewe wala mtu mwingine yeyote.
Kikwete
aliwataka Watanzania wamuunge mkono Rais Magufuli katika jitihada
anazofanya za kukabiliana na wakwepa kodi, huku akitoa mfano akisema
wakwepa kodi kwa Serikali ni kama inzi na kidonda, hawaondoki bila
kufukuzwa na ukiacha kuwafukuza wanarudi.
“Serikali
ina wajibu kwa wananchi, wanataka barabara, shule, hospitali ziwe na
dawa na mengine mengi, lakini haya yote yanahitaji fedha na Serikali
inapata fedha kutoka katika vyanzo vya kodi,” alisema.
Alisema
pia yapo mapato mengine ikiwemo ushuru mbalimbali kama katika kulipia
leseni, hati za kusafiria na nyingine, lakini pia Serikali inaweza
kuchukua mikopo na misaada.
Kikwete
alisisitiza kuwa wakati wa uongozi wake, kazi hiyo ya kuongeza
ukusanyaji wa mapato na kuziba mianya ya upotevu wa mapato ilifanyika,
ndio maana alifanikiwa kuongeza makusanyo ya kodi kutoka Sh bilioni 177
kwa mwezi mpaka Sh bilioni 900.
Pamoja
na mafanikio hayo ya uongozi wake, Kikwete alisema bado mahitaji ya
Serikali kwa watu wake, yameendelea kuwa makubwa kuliko upatikanaji wa
mapato.
“Tunapaswa
kuendelea kuboresha mifumo ya kodi, taasisi za mapato na kupata
watendaji waadilifu, kwa kuwa kama mifumo na taasisi vikiwa imara,
lakini watendaji si waaminifu haisaidii.
Alisema
kazi hiyo anayofanya Dk Magufuli ni kubwa kwa kuwa inahusisha
kunyang’anya tonge watu na kusisistiza namna bora ya kumuunga mkono ni
kulipa kodi na wakusanyaji wa mapato ya Serikali wawe waaminifu.
Kikwete
ambaye ni Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, alisema hata katika kikao cha
Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho walichokaa
juzi, waliamua kumuunga mkono Rais Magufuli na kuwataka wanachama wote
wa chama hicho kufanya hivyo.
“Ni
pale tu mapato yatakapoongezeka, ndipo wajibu wa Serikali katika
kuhudumia wananchi utawezekana, tukimuunga mkono Rais wetu mzuri ataweza
na mapato yakiongezeka, maji yatapatikana, mapato yakiongezeka,
zahanati na hospitali zetu zitapata dawa za kutosha, mapato yakiongezeka
barabara za lami zitajengwa,” alisisitiza.
Alisema
katika Serikali Kuu, makusanyo yako nyuma ya asilimia 10 ya lengo,
lakini kwa juhudi za Rais Magufuli, hali inavyokwenda lengo hilo
litapitwa na Serikali itaanza kuzungumzia makusanyo ya matrilioni kwa
mwezi.
Hata
hivyo, alisema juhudi hizo za Serikali Kuu hazionekani katika
halmashauri ambako ni kama hakuna kazi inayofanyika na hata pale
kunapokuwa na juhudi za kukusanya mapato, wakati mwingine yanaishia
mikononi mwa wajanja.
Kikwete
ambaye alifanya usafi katika soko ikiwemo kufagia, kukusanya na kuzoa
taka akiwa na mkewe, huku akikataa kuvaa vifaa vya kuzuia vumbi,
aliwataka wananchi kujenga utamaduni wa kufanya usafi.
Alisema uamuzi wa Rais Magufuli wa
kutumia maadhimisho ya miaka 54 ya Uhuru, kuwataka wananchi wote wafanye
usafi, ni wa busara na si wa kukurupuka kwa kuwa mwaka huu taifa
lilikabiliwa na ugonjwa wa kipindupindu.
No comments:
Post a Comment