Baba awachoma moto wanaye, kisa samaki - LEKULE

Breaking

29 Dec 2015

Baba awachoma moto wanaye, kisa samaki



IMG_20151216_170055
Ester Lucas akiwa na majeraha ya moto mkononi.

NA VICTOR BARIETY, Uwazi

GEITA: Baba mzazi wa watoto wawili, Lucas Petro mwenye umri wa miaka 29, anatafutwa na polisi kwa kosa la kuwachoma moto watoto wake, Denis (5) na Ester Lucas, 3, (pichani) baada ya kuwatuhumu kuiba mboga aina ya samaki kwa jirani yao, tukio lililotokea katika Kijiji cha Msasa, Kata ya Busanda wilayani Geita, mwishoni mwa mwezi Novemba, mwaka huu.


Wakizungumza katika ofisi za mtendaji wa kata kijijini hapo, watoto hao ambao wameunguzwa mikononi, miguuni na midomoni, walisema walifanyiwa vitendo hivyo baada ya baba yao kuwafungia majani kabla ya kuwachoma moto, kwa kitendo chao cha kula mboga yote ya jirani yao, Maneno Balinozya.
IMG_20151216_170238
Denis Lucas akiwa na majeraha mguuni baada ya kuchomwa moto na baba yake.


Ofisa mtendaji wa kijiji hicho, Hamis Mandikilo alidai kuwa watoto hao waligunduliwa Desemba 12, mwaka huu majira ya saa 6 mchana wakati wajumbe wa kamati ya huduma ya jamii walipokuwa wakipita kila kaya kuhamasisha zoezi la usafi wa mazingira.
Alisema baada ya kuwagundua, waliwachukua hadi ofisini kwake na kuamuru mgambo wamkamate baba yao kwa hatua zaidi za kisheria, ambapo walifanya hivyo na kumfikisha ofisini kwake kwa mahojiano zaidi kabla ya kumpeleka polisi.
mikono ya mtoto ester
….Jeraha la Ester.


“Walipomfikisha ofisini kwangu nilimhoji na alikiri kutenda kosa hilo kwa madai kuwa watoto hao walikwenda kwa jirani yao Balinozya na kukomba mboga na ndipo alipoamua kuwafungia majani makavu kisha kuwalipua moto,’’ alisema.
Kufuatia hali hiyo, mtendaji huyo aliamua kumfikisha mtuhumiwa huyo ofisi ya mtendaji wa kata hiyo, Juster Mabala ambako alishikiliwa kwa siku mbili mfululizo hadi alipowatoroka walinzi wa ofisi hiyo na kutokomea kusikojulikana.
visigino vya mtoto Denis Wakati polisi wakiendelea kumsaka, watoto hao wanatibiwa katika hospitali ya wilaya kwa gharama za ofisi ya mtendaji wa kata hiyo.

No comments: