Amuua Mwenzake Kwa Kisu Wakigombea Mwanamke - LEKULE

Breaking

3 Jul 2015

Amuua Mwenzake Kwa Kisu Wakigombea Mwanamke

WATU watatu wamekufa katika matukio matatu tofauti katika Wilaya za Tarime na Rorya akiwemo mtu aliyeuawa wakati wanagombania mwanamke.
 
Waliokufa ni Chacha Mwita (24) aliyechomwa kisu kifuani na mwenzake wakigombea mwanamke wa baa huko Sirari. 
 
Wengine ni Juma Nguka (25) aliyeuawa na watu wenye hasira baada ya kutuhumiwa kupora pikipiki yenye namba za usajili MC 936 ACA, mali ya Erick Jumanne mkazi wa Kijiji cha Mkoma.
 
Tukio lingine ni kufa maji kwa mvuvi aliyefahamika kwa jina la Wambura Maregeri (30) mkazi wa kijiji cha Muhundwe aliyekufa maji baada ya Boya kutoboka.
 
Kaimu Kamanda wa Polisi Tarime Rorya ACP Swetbert Njewike alisema kuwa matukio hayo matatu ya vifo yalitokea Julai mosi mwaka huu katika Wilaya za Rorya na Tarime.
 
Akielezea tukio la baa ambalo Mwita aliuawa, alisema siku hiyo marehemu akiwa baa moja katika mji wa Sirari, Tarime, nyakati za saa moja jioni kulitokea ugomvi kati ya marehemu na mtu mwingine ambaye hajafahamika jina lake wakigombania mwanamke aliyetajwa kwa jina moja la Dina.
 
Alisema wakati wa ugomvi huo, Mwita alichomwa kisu kifuani na aliyefanya kitendo hicho alitoroka ambapo majeruhi huyo alitokwa damu nyingi na alipofikishwa Hospitali ya Wilaya Tarime alifariki dunia.
 
Alisema Nguka yeye alipoteza maisha baada ya kushambuliwa na wananchi wenye hasira baada ya kudaiwa kuiba pikipiki. 
 
Akasema Maregesi alikufa maji baada ya boya lililotengenezwa kienyeji alilokuwa anatumia katika uvuvi kutoboka na kuzama majini hali iliyopelekea kifo chake.
 
“Jeshi la Polisi linafanya msako wa watuhumiwa wa mauaji Chacha Mwita na watuhumiwa waliohusika katika mauaji ya Nguka ili waweze kufikishwa katika vyombo vya Sheria,” alisema.
 

Aliwaonya wananchi kutojichukulia sheria mikononi ya kuwauawa watu wengine badala yake wawafikishe katika vyombo husika vikiwemo vya Dola. 
 
 Aliwaomba raia wema kutoa taarifa mara watakapowaona watuhumiwa hao wa mauaji hayo ii wakamatwe.

No comments: