Waziri Mkuu Ataka Amani ya Nchi Ilindwe......Akemea Uvaaji wa Nguo Fupi na Matumizi Ya Dawa Za Kulevya - LEKULE

Breaking

25 Dec 2015

Waziri Mkuu Ataka Amani ya Nchi Ilindwe......Akemea Uvaaji wa Nguo Fupi na Matumizi Ya Dawa Za Kulevya


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wananchi waendelee kulinda amani ya nchi huku akikemea uvaaji wa nguo fupi na kuwasihi Watanzania kujenga tabia ya kuvaa mavazi yenye kumpendeza Mungu.
 
Pia, amekemea matumizi ya dawa za kulevya na mimba za utotoni akisema ni mambo ambayo yanaepukika kwa mtu yeyote aliyelelewa katika misingi ya kidini.
 
Waziri Majaliwa alisema hayo jana alipokuwa akihutubia Baraza la Maulid lililofanyika Karimjee jijini Dar es Salaam.
 
Alisema mambo yote hayo yanawezekana kama watu watamkimbilia Mungu huku akiwaomba viongozi wa dini kuwausia waumini wao kuvaa mavazi ambayo yanampendeza Mungu.
 
“Mtoto akilelewa kwenye mazingira ya dini itakuwa ngumu kuvaa mavazi ambayo hayampendezi Mungu,” alisema.
 
Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za kidini zile ambazo ziko kisheria huku akizitaka ziendelee kuisaidia Serikali kwa kujenga shule na hospitali na kutoa huduma nyingine za kijamii.
 
Waziri Majaliwa alitumia fursa hiyo kuwapongeza Watanzania kwa kuwa watulivu katika kipindi chote cha uchaguzi hadi ulipofanyika Oktoba 25.
 
Akizungumza katika baraza hilo, Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti, Abubakari Zuberi aliwaasa waumini wa Kiislamu kufanya mambo yote yanayompendeza Mwenyezi Mungu.
 

Aliwashukuru Waislamu wote nchini kwa kushirikiana na wananchi wenzao ambao siyo wa dini hiyo katika kudumisha amani. 

No comments: