Serikali Yapiga Marufuku Matangazo Yote Yanayohusu Tiba asili na Tiba Mbadala Kwenye Vyombo vya Habari na Mitandao ya Kijamii. - LEKULE

Breaking

25 Dec 2015

Serikali Yapiga Marufuku Matangazo Yote Yanayohusu Tiba asili na Tiba Mbadala Kwenye Vyombo vya Habari na Mitandao ya Kijamii.


Taarifa kutoka Wizara ya Afya kuanzia tarehe 24 Desemba 2015 imepiga marufuku matangazo yote yanayohusu tiba asili na tiba mbadala kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Wale wote wenye vibali wanatakiwa kuviwasilisha vibali na matangazo yao kwenye Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala ili vifanyiwe mapitio.

Utoaji wa elimu ya afya kwa umma unaofanywa na watoa huduma za tiba asili na tiba mbadala kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii umepigwa marufuku hadi hapo utaratibu mwingine utakapotangazwa.

Watoa huduma za tiba asili na tiba mbadala nchini kote wanaagizwa wawasilishe kwenye Baraza nyaraka zote muhimu ndani ya wiki mbili kuanzia jana Desemba 2015. 

Baadhi ya nyaraka hizo ni zile zinazohusu kuuza dawa za asili na tiba mbadala, nyaraka za kumiliki mashine zinazotumika katika kufanya uchunguzi katika tiba asili na tiba mbadala

Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala linaagizwa katika kipindi cha siku 14 kuanzia jana  24 Desemba 2015, lipitie nyaraka zote  zinazohusu usajili wa watoa huduma, usajili wa vituo vyao, ikiwa ni pamoja na maduka ya dawa za asili na dawa za tiba mbadala, usajili wa dawa zote zinazotumika katika huduma hizo na usajili wa mashine zote zinazotumika katika huduma za tiba asili na tiba mbadala.

Taarifa hii imetolewa na Dismas Lyassa kwa niaba ya Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Dk Hamis Kigwangala na kusainiwa na M.O John, Kaimu Katibu Mkuu.



No comments: