Shambulio katika uwanja wa ndege lauwa watu 41 Istanbul - LEKULE

Breaking

30 Jun 2016

Shambulio katika uwanja wa ndege lauwa watu 41 Istanbul

Washambuliaji wa kujitowa muhanga wamewauwa zaidi ya watu 41 na kujeruhi wengine 140 katika shambulio dhidi ya uwanja wa ndege wa Ataturk mjini Istanbul katika mfululizo wa miripuko ya mabomu dhidi ya Uturuki.
Idadi ya watu waliouwawa katika shambulio la uwanja wa ndege wa Istanbul imeongezeka na kufikia 41. Awali Waziri Mkuu wa Uturuki Binali Yidirm amesema watu 36 wameuwawa hapo jana wakiwemo washambuliaji watatu wa kujitowa muhanga ambao waliwasili katika uwanja wa ndege huo kwa kutumia taxi na kujiripuwa mara tu baada ya kuanza kufyatuwa risasi.Waziri wa sheria wa Uturuki Bekir Bozdag amesema watu 147 wamejeruhiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari katika uwanja wa ndege huo baada ya kutokea kwa shambulio hilo hapo jana Waziri Mkuu wa Uturuki Binali Yidrim amesema kundi la Dola la Kiislamu linaonekana kuhusika na shambulio hiilo
Binali amesema "Uchunguzi wa vikosi vyetu vya usalama unaashiria kwamba shambulio hilo la kigaidi limetekelezwa na kundi la Daesh na licha ya kwamba uchunguzi unakielekezea kidole kundi hilo la Dola la Kiislamu uchunguzi huo bado unaendelea.Uwanja wa ndege unafunguliwa tena kwa safari saa nane usiku na safari za ndege zitarudi katika hali ya kawaida."
Kwa mujibu wa maafisa polisi ilifyatuwa risasi kujaribu kuwazuwiya washambuliaji wawili kabla hawajafika kituo cha ukaguzi wa usalama katika ukumbi wa kuwasili abiria katika uwanja wa ndege huo lakini waliripuwa mabomu yao. Afisa wa Uturuki amesema wengi waliouwawa walikuwa ni raia wa Uturuki lakini pia kuna wageni miongoni mwa watu waliouwawa.
Shambulio lafanana na la Brussels
Shambulio hilo kwa kiasi fulani linafanana na shambulio la kujitowa muhanga lililofanywa na wanamgambo wa kundi la Dola la Kiislamu katika uwanja wa ndege wa Brussels hapo mwezi wa Machi na kuuwa watu 16 kabla ya shambulio jengine kuuwa watu wengine 16 siku hiyo hiyo katika njia ya reli ya chini ya ardhi katika mji mkuu huo wa Ubelgiji.
Mashahidi walirepoti kusikia milio ya risasi kutoka sehemu mbali za uwanja wa ndege huo wa Atartuk ambao ndio uwanja wa ndege mkubwa kabisa nchini Uturuki na wa tatu kwa kuwa na harakati kubwa za safari za kimataifa barani Ulaya.
Rais Recep Tayyip Erdogan amelani shambulio hilo la kigaidi dhidi ya raia wasiokuwa na hatia.
Uwanja wafunguliwa tena
Ndege tayari zimeanza kutuwa tena katika uwanja wa ndege huo leo ajafiri baada ya uwanja wa ndege huo kufungwa kabisa kwa masaa kadhaa hapo jana kufuatia shambulio hilo la kigaidi.Mamia ya safari zilifutwa kufuatia shambulio hilo.
Shirika la ndege la Uturuki ambalo limefuta zaidi ya safari 340 limekuwa likiwarejeshea abiria fedha zao au tiketi mbadala lakini bado kuna mkanganyiko kwa wasafiri wengi.
Shambulio hilo la jana ni baya kabisa kuwahi kushuhudiwa nchini humo kwa zaidi ya muongo mmoja mjini Istanbul.Kundi la Dola la Kiislamu limekuwa likilaumiwa kwa kuhusika na mashambulio kadhaa nchini Uturuki katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.DW

No comments: