Mapigano makali kusini mwa Burundi - LEKULE

Breaking

30 Jun 2016

Mapigano makali kusini mwa Burundi

media
Askari wa Burundi wakipiga doria katika mitaa ya Bujumbura, baada ya shambulio la guruneti, Februari 3, 2016.
Mapigano makali yanaripotiwa tangu Alhamisi hii Asubuhi katika kijiji cha Mubuga mtaa wa Gasanda, mkoani Bururi, kusini mwa Burundi. Mapigano hayo ni kati ya vikosi vya usalama vikishirikiana na jeshi na kundi la waasi.
Mpaka sasa hasara kufuatia mapigano hayo haijajulikana, lakini chanzo cha polisi kinabaini kwamba mpiganaji mmoja ameuawa na watu wawili wamejeruhiwa, huku wapiganaji watano wakikamatwa na silaha zao.
Kiongozi wa vijana wakereketwa wa chama madarakani (Imbonerakure) na askari polisi wamejeruhiwa kwa mujibu wa mkuu wa mkoa wa Bururi, Christian Nkurunziza.
“Mapema asubuhi tulipata taarifa kwamba kuna kundi la majambazi 11 wenye silaha ambao walikua katika kijiji cha Mubuga, vikosi vya usalama viliwaona na kuanza kupambana nao”, amesema mkuu wa mkoa wa Bururi, akihojiwa kwa njia ya simu na RFI.
“Jambazi mmoja ameuawa na wengine watano wamekamatwa”, Christian Nkurunziza ameongeza.
Jambazi au majambazi ni neno linalotumiwa mara kwa mara na serikali, ikimaanisha wapiganaji wa makundi ya waasi yaliyoanzishwa baada ya maandamano dhidi ya muhula wa tatu wa Rais Pierre Nkurunziza.
Kwa mujibu wa shahidi ambaye hakutaka jina lake litajwe, “askari polisi mmoja na kijana kutoka kundi la vijana wa chama madarakani (ambao Umoja wa Mataifa unawaita wanamgambo) wamejeruhiwa”.
Mkuu wa mkoa wa Bururi amebaini kuhusu kijana huyo kutoka kundi la vijana wa chama tawala (Imbonerakure) kwamba “mtu aliyejeruhiwa ni raia wa kawaida ambaye alikua aliitikia wito wa serikali wa kushirikiana na vikosi vya usalama kwa kuwakamata majambazi hao.”
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Mubuga wameyatoroka makazi yao na wengine wamesema kuwa na hofu ya kuwa huenda mapigano hayo yakachukua muda mrefu.
Mapigano hayo yanatokea wakati ambapo serikali ya Bujumbura imekua ikibaini kwamba tayari imerejesha hali ya utulivu nchini kote.
Hata hivyo hali ya usalama imeendelea kudorora katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo, ambapo magruteni na mauaji ya kuvizia au visa vya ulipizaji kisasi vimekua vikiripotiwa.
Machafuko nchini Burundi yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 500, kwa mujibu wa mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu na zaidi ya watu 270,000 kukimbilia nje ya nchi kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi (UNHCR).RFI

No comments: