Mwenyekiti wa Kitongoji Auawa Baada ya Kufumaniwa Akifanya Mapenzi na Mke wa Mtu Vichakani - LEKULE

Breaking

1 Apr 2016

Mwenyekiti wa Kitongoji Auawa Baada ya Kufumaniwa Akifanya Mapenzi na Mke wa Mtu Vichakani


Mwenyekiti wa Kitongoji cha Bweya katika Kijiji cha Bweya mkoani Geita, Augustine Katemi (42) ameuawa baada ya kufumaniwa akifanya mapenzi na mke wa mtu vichakani.

Mwenyekiti huyo alifariki dunia papohapo baada ya kudaiwa kushambuliwa kwa sime na mume wa mwanamke huyo, mkazi wa Kijiji cha Luchili, Wilaya ya Buchosa mkoani Mwanza.

Tukio hilo lilitokea saa nne usiku Machi 28 baada ya marehemu kudaiwa kukutwa akifanya tendo la ndoa na Chausiku Isangula (32).

Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Latson Mpojoli alisema  hana za taarifa za tukio hilo na kuahidi kufuatilia.

Ilielezwa kuwa Katemi aliuawa baada ya kushambuliwa kwa sime na kufa papohapo na baada ya tukio hilo, mtuhumiwa anadaiwa kumshambulia mkewe kwa kutumia sime hiyohiyo na kumsababishia majeraha makubwa sehemu mbalimbali za mwili na amelazwa kwenye Kituo cha Afya cha Nzera.

Mtendaji wa Serikali ya Kijiji cha Bweya, Samson Walwa alisema baada ya kutokea tukio hilo wananchi waliendesha msako na kumtia mbaroni mtuhumiwa wakati akijaribu kutoroka kuelekea Sengerema.

Walwa alisema mtuhumiwa alikamatwa nyumbani kwa Edward Iswalala alipokuwa amefikia kwa siri kutoka Luchili ili kufuatilia mwenendo wa mkewe ambaye anadaiwa kuwa awali alimuaga kuwa anakwenda kumsalimia baba yake mzazi anayetibiwa kwa mganga wa kienyeji.

“Inavyosemekana alikuwa akifuatilia mienendo ya mke wake… sisi tulipomkamata tumemkabidhi Kituo cha Polisi cha Nzera pamoja na nguo za marehemu (mwenyekiti) na zile za mkewe kwani alipofanya mauaji hayo alizichukua nguzo zao hadi tulipomkata nazo,” alisema Walwa.

Mmoja wa wananchi walioshuhudia tukio hilo, Jumanne Tole alisema, Chausiku alimuaga mumewe kuwa alikuwa anakwenda kijiji cha Kalebezo kumsalimia baba yake mzazi kwa waganga wa tiba asilia alikokuwa anatibiwa lakini baada ya kufika na kumsalimia, alikwenda kwa kaka yake aitwaye Ndagabwene Isangula huko Bweya alikofikwa na mkasa huo.


Alisema kuna madai kuwa mtuhumiwa alifika kijijini hapo kwa siri akiwa amevaa nguo na kofia zilizochakaa ili asifahamike wakati akifuatilia nyendo za marehemu na mkewe na akafanikiwa ikidaiwa kwamba alikuwa na watu ambao walikuwa wakimpatia taarifa hizo. 

No comments: