MURO: TFF ITUMIE BUSARA KABLA YA COASTAL UNION VS YANGA FA CUP - LEKULE

Breaking

14 Apr 2016

MURO: TFF ITUMIE BUSARA KABLA YA COASTAL UNION VS YANGA FA CUP

IKIIBUKA na ushindi katika mchezo wake wa Jumatano hii katika ligi kuu Tanzania Bara (VPL,) dhidi ya Mwadui FC katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaan, timu ya Yanga SC imefurahia kupangwa na Coastal Union katika hatua ya nusu fainali ya kombe la FA.

Mkuu wa kitengo cha habari wa klabu hiyo, Jerry Murro kwa upande mwingine amelalamikia muda mfupi wa timu yake kutoka Misri na kurejea nchini kucheza na Coastal, April 24.

“Tunashukuru tumeweza kujua mshindani wetu ni nani na tutacheza wapi mchezo wetu wa nusu fainali katika kombe la FA. Hiyo ni hatua ya kwanza, hatua ya pili sasa ni kutayarisha kikosi ili tuwezekuwa na wakati mzuri kuhakikisha tunafanya vizuri kwenye michuano hii”, anasema Muro akizungumzia timu yake kupangwa na Coastal.

“Lakini jambo lingine ambalo linaonekana kututatiza ni ratiba. Ratiba inaonesha tutacheza tarehe 24 na sisi tutakuwa na mchezo wa klabu bingwa nchini Misri tarehe 20. Tutarejea tarehe 21 usiku wa kuamkia tarehe 22. Tarehe 23 itatupasa kusafiri kuelekea Tanga halafu tarehe 24 tucheze mchezo.”

“Sisi tunadhani kwa kuwa michuano hii ni yetu sisi watanzania na tuna timu mbili katika michuano ya CAF. Azam FC wenzetu wanacheza tarehe 21 huko Tunisia na wote (Yanga na Azam) tupo katika michuano hii (FA), tunadhani ni busara kwa Shirikisho la mpira nchini (TFF) watupe muda kidogo ili tuweze kujipanga.”

“Ikumbukwe mchezo wetu wa FA utachezwa katika uwanja wa Mkwakwani japo hicho kinaweza kisiwe kigezo sana lakini hoja yetu ya msingi, tunarudi kutoka Misri tarehe 21 usiku, tunadhani siku mbili kusafiri Dar kwenda Tanga na kuanza mchezo wetu tarehe 24 sidhani kama ni jambo zuri.” anamaliza kusema Murro. 

No comments: