Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla aagiza hekta 5,000 zirejeshwe kwa wananchi - LEKULE

Breaking

7 Apr 2016

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla aagiza hekta 5,000 zirejeshwe kwa wananchi


Mkuu  wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla ameamuru hekta 5,000 za ardhi zilizokuwa za Chama cha Ushirika cha Luhanga Amcos zirejeshwe kwa wananchi wa kijiji cha Luhanga wilayani Mbarali kutokana na mchakato wa kutoa ardhi hiyo kuwa batili.

Makala alitoa agizo hilo jana mbele ya wakazi wa kijiji cha Luhanga, katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo, huku akimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbarali, Jeremiah Mahinya kuwachukulia hatua viongozi wa kijiji waliohusika kutoa ardhi hiyo.

“Ardhi hiyo sasa ni ya wananchi kwa kuwa mchakato uliofanyika ni batili na lazima Mkurugenzi uchukue hatua dhidi ya yeyote aliyehusika kwenye mchakato huu. Iwe alighushi mihtasari au alifanya nini lazima achukuliwe hatua”, alisema.

Alisema wanachama wa Luhanga Amcos walikubaliana na kijiji hicho kupewa ekari 800 za ardhi kwa ajili ya shughuli za kilimo na wao kuahidi kuwa watasaidia kutatua tatizo la maji lililokuwa likiwakabili wakazi wa kijiji hicho ambao ni wakulima na wafugaji.

Hata hivyo, ilielezwa kuwa baadaye nyaraka zilibadilishwa na kubainisha kuwa ardhi waliyopewa wawekezaji hao ni hekta 5,000, hatua iliyoleta mkanganyiko na malumbano baina ya wananchi, uongozi wa kijiji na wawekezaji.

Alisema pamoja na malalamiko ya ongezeko kubwa la ardhi pia wawekezaji hao hawakutimiza ahadi ya kupeleka maji hadi sasa wakati wao wameanza kutumia sehemu ya ardhi waliyopora kwa kijiji hicho.

Makalla alisema, kurejeshwa kwa hekta 5,000 za ardhi kwa wananchi kunazingatia vigezo muhimu kikiwemo cha kijiji kutoruhusiwa kuuza au kutoa ardhi inayozidi ekari 50 kwa mtu yeyote sambamba na kutotimizwa kwa ahadi ya kupelekwa maji kijijini hapo.

Alisema kwa sasa serikali inahimiza kila mtu kujituma katika kazi lakini iwapo hakuna maeneo kwa ajili ya shughuli za kilimo vijana watakuwa wanaonewa pale inaposisitizwa kaulimbiu ya Hapa Kazi Tu.


Aliitaja wilaya ya Mbarali kuwa miongoni mwa maeneo yanayoongoza kwa migogoro mingi ya ardhi aliyosema mingine ni ya kujitakia au ile inayotokana na watendaji kutosikiliza wananchi.

No comments: