KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA KILIMO,MIFUGO NA MAJI YARIDHISHWA NA MATUMIZI YA FEDHA MTAMBO WA RUVU CHINI - LEKULE

Breaking

3 Apr 2016

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA KILIMO,MIFUGO NA MAJI YARIDHISHWA NA MATUMIZI YA FEDHA MTAMBO WA RUVU CHINI


Meneja wa Mtambo wa Maji wa Ruvu Chini Mhandisi Emmanuel Makusa (katikati) akiwaongoza Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kutembelea Mtambo wa Maji wa Ruvu Chini,wilayani Bagamoyo kujionea maendeleo yaliyofikiwa kufuatia kukamilika kwa ujenzi wa bomba lenye urefu wa Kilometa 56 linalotoka katika mtambo huo kwenda jijini Dar es salaam.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakiangalia sehemu ya kukusanyia maji kutoka mto Ruvu kwenye Mtambo wa Ruvu Chini.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakiangalia mitambo ya kuchujia maji kutoka mto Ruvu kwenye Mtambo wa maji wa Ruvu Chini.
Meneja wa Mtambo wa Maji wa Ruvu Chini Mhandisi Emmanuel Makusa akitoa ufafanuzi kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji namna chumba cha kuongozea mitambo ya Ruvu chini kinavyofanya walipotembelea Mtambo wa Ruvu Chini,wilayani Bagamoyo kujionea maendeleo yaliyofikiwa kufuatia kukamilika kwa ujenzi wa bomba lenye urefu wa Kilometa 56 linalotoka katika mtambo huo kwenda jijini Dar es salaam.
Meneja wa Mtambo wa Maji wa Ruvu Chini Mhandisi Emmanuel Makusa akizungumza jambo na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Mhe. Mary Nagu wakati kamati hiyo ilipotembelea Mtambo wa Ruvu Chini,wilayani Bagamoyo .
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ( katikati) na baadhi ya wajumbe wakimsikiliza kwa makini Meneja wa Mtambo wa Maji wa Ruvu Chini Mhandisi Emmanuel Makusa mara baada ya kutembelea sehemu ya kuchujia maji na kuchanganyia dawa.

Sehemu ya kuchujia maji katika mtambo wa Ruvu Chini.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakiangalia eneo lenye pampu za kusukumia maji kutoka mtambo wa Ruvu Chini kwenda matangi ya maji yaliyoko Chuo Kikuu Ardhi jijini Dar es salaam.
Eneo la kukusanyia maji kutoka mto Ruvu kwenda kwenye mtambo wa kusafishia Maji.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kukamilisha ziara ya kutembelea mtambo wa kuzalisha maji wa Ruvu Chini, Bagamoyo mkoani Pwani. Picha zote na Aron Msigwa - MAELEZO.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji imeridhishwa na matumizi ya fedha kiasi cha shilingi Bilioni 141 zilizotolewa na Serikali kugharamia mradi mkubwa wa ujenzi wa bomba la maji kutoka Mtambo wa Ruvu Chini,wilayani Bagamoyo kwenda jijini Dar es salaam kufuatia ujenzi wake kukamilika.

Akizungumza mara baada ya Kamati hiyo kutembelea maeneo mbalimbali ya mradi huo ikiwemo mtambo wa Maji wa Ruvu Chini ulioko Bagamoyo mkoani Pwani, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Hanan'g Mhe. Mary Nagu amesema kuwa kamati kamati yake imeridhishwa na ubora wa kazi iliyofanyika chini ya Usimamizi wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es salam ( DAWASA).

Amesema mradi huo wenye urefu wa kilometa 56 umekamilika na kueleza kuwa itakua historia kwa wananchi wa Dar es salaam waliounganishwa na mtandao wa mabomba ya DAWASCO kukosa maji.

Amesema kama kamati wamejiridhisha kuwa kiasi cha maji kinachozalishwa kwa siku lita milioni 270 kutoka mtambo wa Ruvu Chini ni kingi na kueleza kuwa kiwango hicho kitaongezwa kwenye uzalishaji wa awali.

"Sisi kama Kamati ya Bunge tumeridhishwa na kazi nzuri iliyofanyika, tumeshuhudia wenyewe maji yanayozalishwa ni mengi tunaipongeza Serikali kwa kusikia kilio cha muda mrefu cha wakazi wa jiji la Dar es salaam" Amesema Mhe.Nagu.

Amesema kazi iliyopo sasa kwa Serikali na mamlaka zinazohusika ni kuhakikisha kuwa inakabiliana na na changamoto ya usambazaji wa maji hayo ili wakazi wengi zaidi wa jiji hilo wanaunganishwe na mtandao wa mabomba ya DAWASCO.

Amewataka DAWASCO kuifanya kazi hiyo kwa kasi pia kuangalia upya gharama za usambazaji wa maji pia kuwaangalia upya mawakala waliowekwa kusimamia usambazaji wa maji ili kuwadhibiti wale wasiowaaminifu ili wananchi waweze kupata maji kwa bei nafuu na kuepuka kutumia maji yasiyo salama ambayo yamekuwa chanzo cha milipuko ya magonjwa ikiwemo kipindupindu.

Aidha,ametoa wito kwa wananchi kulinda na kutunza vyanzo vya maji ili upatikanaji wa maji hayo uwe endelevu huku akitoa wito kwa Wizara kulifanyika kazi suala la kuwapatia maji wananchi wote wanaoishi kuzunguka miundombinu mikubwa ya maji kote nchini ili kuimarisha ulinzi na usalama.

Kwa upande wake Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge akizungumza mara baada ya kukamilika kwa ziara ya wabunge hao kwenye mtambo wa Maji wa Ruvu Chini amesema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutalifanya jiji la Dar es salaam kupata maji.

Amesema katika kuchukua hatua za kukabiliana na uhaba wa maji Serikali iliamua kufanya maboresho makubwa mifumo ya maji kwa kujenga mipya na kurekebisha ile ya zamani ili kuendana na kasi ongezeko la uhitaji wa maji.

Amesema kazi kubwa ambayo inaendelea sasa ni kuhakikisha usambazaji katika maeneo yenye mitandao ya mabomba na ile ambayo haikuwa na mitandao ya mabomba ili kuwapatia maji ya uhakika.

" Naishukuru kamati kwa kuja kutembelea mradi wetu wametupa changamoto ya kuhakikisha maji yanafika kwa wananchi, sisi kama serikali tuna mpango wa kuhakikisha tunaondoa mifumo yote chakavu katika jiji la Dar es salaam kwa kuweka mipya na hii tunaendelea nayo kwa kasi" Amesisitiza.

Amesema kazi ya kuweka miundombinu ya usambazaji maji katika jiji la Dar es salaam imeshaanza akifafanua kuwa Serikali imeingia mikataba na wakandarasi kuhakikisha kuwa kazi hiyo inafanyika kwa viwango.

Aidha, amesema kuwa baadhi ya maeneo ya jiji ikiwemo eneo la Kimara kazi inaendelea huku maeneo ya katikati ya jiji miundombinu yake ni chakavu inaendelea kubadilishwa ili iweze kuhimili wingi na nguvu ya maji inayosukumwa

Ametoa wito kwa wananchi na wenye viwanda kutumia maji hayo ili kulinda afya za walaji kwa kuwa maji hayo ni salama na yamepita kwenye vipimo vya ubora ili kuepuka kutumia maji yasiyo salama ambayo yamekuwa chanzo cha magonjwa.

" Tumeshatoa maelekezo viwanda vyote vya Dar es salaam vihakikishe kuwa vinatumia maji haya, sasa tuna maji ya kutosha, waje tuwaunganishe na maji haya japo baadhi yao wamekuwa wakijiunganishia maji kiholela na kutumia visima wanavyochimba ambavyo si salama".

Kuhusu Serikali kuhakikisha ulinzi wa mtandao wa bomba hilo lenye urefu wa Kilometa 56 amesema kuwa kazi hiyo inafanywa na DAWASCO ikiwahusisha viongozi na wananchi ambao mradi unapita katika maeneo yao.

" Ni kweli ulinzi wa bomba hili ni muhimu,DAWASA wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi katika maeneo linakopita bomba, pia tumeshaweka matoleo kwa ajili ya kuhakikisha tunawafikishia huduma ya maji wananchi wanaoishi kuzunguka bomba hili ili nao wawe sehemu ya walinzi wa mradi wao" Amesema.

Mhe. Lwenge ameongeza kuwa Shirika la Maji Safi na Maji Taka Dar es salaam (DAWASCO) litaweka mfumo wa ulinzi wa kieletroniki ili kulinda bomba hilo, mfumo huo utakua unapima kiwango cha msukumo wa maji yanayotoka Ruvu Chini kisha kutoa taarifa kwenye vituo vitakavyoanzishwa endapo itatokea hitilafu ya miundombinu hiyo.

Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo ambao ni Wabunge wakizungumzia kukamilika kwa mradi huo wamesema kuwa wameridhishwa na kazi kubwa iliyofanywa na serikali na kwamba itaondoa kero ya maji katika jiji la Dar es-slaam.

Mbunge wa jimbo la Itirima, Mhe. Njalu Silanga ambaye ni mmoja wa wajumbe wa Kamati hiyo ameeleza kuwa ameridhishwa na kazi nzuri iliyofanywa na Serikali kwa kuwa mradi huo umejengwa katika viwango vya hali ya juu na kuongeza kwamba wakazi wa Dar es salaam sasa watarajie kupata maji Safi na Salama.

"Naipongeza sana Serikali kwa kufanikisha mradi huu,kweli wamefanya kazi kubwa sana, mimi na wabunge wenzangu tumeona na tumeridhishwa na utendaji wa Serikali katika kuhakikisha jiji la Dar es salaam linapata maji safi na salama"

Ameiomba Serikali kuweka msisitizo katika uimarishaji wa miundombinu ili kuwezesha maji kufika kwa urahisi katika makazi ya watu.

Naye Mhe. Dkt.Sware Semesi, Mbunge wa viti maalum mkoa wa Dodoma akiuzungumzia mradi huo amesema kuwa ameridhishwa na miundombinu imara iliyojengwa na kuiomba serikali kusimamia usambazaji wa huduma hiyo kwa wananchi.

" Mimi pamoja na wabunge wenzagu tumeshuhudia mradi huu ni mkubwa,kilichobaki kwa mamlaka zinazohusika ni kujipanga na kuhakikisha kunakuwa na mgawanyo mzuri wa maji haya,kufanyika kwa Uhakiki na ukusanyanji wa ankara za wateja unaoendana na matumizi halisi ya maji hayo ili huduma hii iwe endelevu" Amesema.

Aidha, ametoa wito kwa DAWASCO kusimamia kikamilifu usambazaji wa lita milioni 270 zinazozalishwa kwa siku na mtambo wa Ruvu chini kwenda matangi ya maji yaliyoko Chuo Kikuu Ardhi 

No comments: