WAZIRI MKUU ATUMA MAWAZIRI WATATU KUTATUA MIGOGORO YA ARDHI SIMIYU - LEKULE

Breaking

6 Mar 2016

WAZIRI MKUU ATUMA MAWAZIRI WATATU KUTATUA MIGOGORO YA ARDHI SIMIYU


mpn1
Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa akifungua jengo la Maabara la Shule ya Sekondari ya Mwakaluba katika jimbo la Kisesa  akiwa aktika ziara ya mkoa wa Simiyu  Machi 5, 2016.   Kulia ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Simiyu , Dkt Titus Kamani na Wazpili kulia ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, J. Mpina. (picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
mpn2
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akikagua maabara ya Shule ya Sekondari ya   Mwakalubi katika jimbo la Kisesa akiwa katika ziara ya mkoa wa Simiyu Machi 5, 2016 (picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
mpn3
Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa akikagua shamba la pamba la mfano la mkulima  Gamuga Kimali  kqtika kijiji cha Nandoya wilayani Meatu akiwa katika ziara ya mkoa wa Simiyu Machi 5, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
mpn6
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipongeza Mama Anastazia Petro kwa kujifungua salam motto wa kiume aliyepewa jina la Majaliwa  wakati alipotembelea Kituo cha Afya cha Mwandoya akiwa katika ziara ya mkoa wa Simiyu Machi 5, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
mpn7
Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa akiteta na Waganga na wauguzi wa Kituo cha Afya cha  Mwandoya wilayani Meatu akiwa katika ziara ya mkoa wa Simiyu Machi 5, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
mpn8
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Madaktari na Wauguzi wa Kituo cha Afya cha Nandoya wilayani Meatu baada ya kuzindua jengo la upasuaji na kusalimia wagonjwa akiwa katika ziara ya mkoa wa Simiyu Machi 5, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema atawatuma mawaziri watatu waje mkoa wa Simiyu ili wakae na uongozi wa kila wilaya pamoja na wananchi ili kubaini tatizo la mipaka baina ya wilaya hizo na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Machi 5, 2016) wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa vijiji vya Mwakaluba na Mwandoya akiwa kwenye siku ya tano ya ziara yake mkoani Simiyu.
“Tangu niingie hapa mkoani malalamiko ya mipaka nimeyapokea kila mahali nilikopita. Nimeamua kuwatuma mawaziri watatu ambao ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. William Lukuvi; Waziri wa Maliasili ua Utalii, Profesa Jumanne Maghembe na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Bw. George Simbachawene waje mkoa huu kutatua matatizo yenu,” alisema.
“…Nitawatuma waje na wapite kila wilaya, wakae na kuzungumza na wakulima na wafugaji ili kubaini ni chanzo cha tatizo la migogoro hii kwenye mipaka ya vijiji na hifadhi ya Serengeti. Pia Waziri wa TAMISEMI itabidi atoe ufafanuzi kuhusu agizo lao la kutofanya shughuli yoyote mita 60 kutoka kwenye mto Simiyu ili wananchi waelewe,” alisema.
Mapema, Mbunge wa Kisesa ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nchi (OMR – Mazingira) alimweleza waziri Mkuu mbele ya wananchi hao kwamba limetolewa zuio linalowakata wakazi wa mkoa huo wasifanye shughuli zozote umbali wa mita 60 kutoka kwenye kingo za mto huo.
“Limebandikwa tangazo linalokataza wananchi waishio kando ya mto Simiyu wasifanye chochote kuanzia Julai 30, 2016. Wananchi hawajashirikishwa wala kuelezwa chochote zaidi ya kuona bango la matangazo tu. Watu wananakatazwa wasichote maji wala kunywesha mifugo wakati hakuna mabwawa, itawezekanaje? Tunaomba kauli yako kuhusu jambo hili,” alisema.
Ili kumaliza tatizo la migogoro ya ardhi hapa nchini, Waziri Mkuu alisema Serikali ina mpango wa kuunda mabaraza ya ardhi 100 kwa nchi nzima ambayo yatakuwa na jukumu la kutatua migogoro ya ardhi kwa wakati
Akitoa taarifa ya wilaya hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Bw. Erasto Sima alisema wilaya hiyo iliyoanzishwa Julai mosi, 1987 ina ukubwa wa kilometa za mraba 8,835 ambapo asilimia 49 (sawa na kilometa za mraba 4,329) ya eneo lote la wilaya hiyo ni hifadhi za wanyamapori.
Alilitaja eneo hilo kuwa ni pori la akiba la Maswa, sehemu ya hifadhi ya Serengeti, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na pori la hifadhi ya usimamizi wa wanyama (WMA) la Makao na kwamba asilimia 51 iliyobakia indiyo inayotumiwa kwa makazi ya watu, kilimo na malisho ya mifugo.

No comments: