Wauguzi sita Temeke wasimamishwa Kazi kwa kuuza gloves - LEKULE BLOG

Breaking

Header Ads

Wednesday, 2 March 2016

Wauguzi sita Temeke wasimamishwa Kazi kwa kuuza gloves


Naibu Waziri wa Afya, Dk Hamis Kigwangalla amewasimamishwa kazi wauguzi sita katika hospitali  ya  Temeke kwa kosa la kuomba rushwa.

Wauguzi waliosimamishwa ni Hadija Salum, Beatrice Temba, Agnes Mwampashe, Elizabeth Mwilawa, Mariam Mohamed na Marion Said, ambao walikuwa zamu katika wodi ya wajawazito wakati wa tukio hilo.

“Nimewasimamisha kazi wauguzi wote waliokuwa zamu jana (juzi) asubuhi, nakuagiza Msajili wa Baraza la Wauguzi uwasimamishe hadi utakapowasafisha kupitia kamati ya msajili,” alisema Dk Kigwangalla.

Mmoja wa wajawazito, Loshan Seif alisema alipowasili juzi asubuhi kwa ajili ya kujifungua, muuguzi mmoja wa zamu alimtaka kulipia Sh5,000 za gloves.

“Siku zote huwa natumia bima lakini jana (juzi) wakaniambia hawatumii, nitoe Sh5,000 za gloves, baadaye niliambiwa natakiwa kuwa na uzi wa mshono, sindano na vingine hivyo kama sina nitoe fedha,” Seif.

Dk Kigwangalla alifanya ziara ya ghafla hospitalini hapo jana saa 9.00 alasiri.

Akizungumza jana alasiri baada ya kufanya ziara ya ghafla Hospitalini hapo na kupata malalamiko hayo kutoka kwa wanawake waliojifungua.

“Mama anaambiwa atoe fedha ya gloves Sh5,000 wakati dukani zinauzwa Sh1,000, nataka liwe fundisho kwa wote wanaotuongezea vifo vya wajawazito kwa tamaa ndogondogo,” alisema Kigwangalla.

Katika ziara hiyo, Dk Kigwangalla alishuhudia ubovu wa vyumba viwili vya upasuaji na kutoa maelekezo kwamba, virekebishwe ndani ya miezi sita.


“Hali ni mbaya ndani ya hizi ‘theater’ zote mbili zifanyiwe ukarabati iwapo itashindikana nitazifunga, lazima ziwe na hadhi yake na nitakuja kukagua,” alisema. 
Post a Comment