TRA Yamdai Profesa Tibaijuka Milioni 500 za Escrow - LEKULE

Breaking

5 Mar 2016

TRA Yamdai Profesa Tibaijuka Milioni 500 za Escrow



Hatima ya kesi ya Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka kupinga kuilipa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zaidi ya Sh500 milioni kutoka katika mgawo wa Sh1.62 bilioni zinazohusishwa na fedha zilizochotwa Akaunti ya Tegeta Escrow, itajulikana Machi 29, wakati Bodi ya Rufaa za Kodi (Trab) itakapotoa uamuzi.

Tarehe hiyo imepangwa na Makamu Mwenyekiti wa Trab, Hakimu Agusta Mmbando baada ya kukamilika kwa hatua ya usikilizwaji pande zote mbili kwenye kesi hiyo.

Profesa Tibaijuka alikata rufaa Trab baada ya TRA kumpelekea madai ya malipo ya kodi ya Sh586 milioni kutokana na mgawo wa Sh1.62 bilioni anazodaiwa kupokea kutokana na fedha zilizochotwa kutoka akaunti hiyo iliyofunguliwa na Shirika la Umeme (Tanesco) na kampuni ya kufua nishati hiyo ya IPTL kwa ajili ya kuhifadhi fedha za malipo ya ununuzi wa umeme wakati mzozo wao ukiwa mahakamani, lakini zikachotwa kwa njia ambayo ilizua shaka.

Rufaa hiyo ilisikilizwa na Hakimu Mmbando Februari 17, 19 na 22 wakati Profesa Tibaijuka alipokuwa akitoa ushahidi.

Inadaiwa kuwa Profesa Tibaijuka, ambaye aliondolewa katika wadhifa wake wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutokana na sakata hilo, aliwekewa fedha hizo kwenye akaunti yake na James Rugemalira, Mkurugenzi wa VIP Engineering & Marketing Limited iliyokuwa kati ya wanahisa wa IPTL.

Kutokana na mgawo huo, Desemba 31, 2015, TRA ilimtaka alipe kodi hiyo, baada ya kushindwa kufanya marejesho kutokana na mgawo huo.

Hata hivyo, alipinga madai hayo na kisha akakata rufaa Trab kupinga hatua ya TRA kumtaka alipe kiasi hicho cha kodi, pamoja na mambo mengine akidai kuwa hajawahi kupokea fedha hizo kutoka kwa Rugemalira.

Katika rufaa hiyo namba 22 ya mwaka 2015, Profesa Tibaijuka anadai kuwa makadirio hayo ya TRA ya malipo ya kodi ni kinyume cha Sheria ya Kodi na hakupaswa kufanya marejesho kwa kuwa hakupokea kipato chochote katika muda huo uliotajwa.

Akiongozwa na wakili wake, Dk Nshalla Rugemeleza wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, Profesa Tibaijuka alidai kuwa fedha hizo zilikuwa ni mchango uliotolewa kwa Taasisi ya Joha Trust, kwa ajili ya Shule ya Wasichana ya Barbro Johansson inayomilikiwa na taasisi hiyo.

Profesa Tibaijuka alidai kuwa yeye si mwanahisa wa taasisi hiyo, bali ni mmoja wa wadhamini na kwamba TRA ilipuuza ushahidi wake kuwa VIP ilitoa mchango kwa Joha Trust na yeye kama mdhamini alizipeleka Joha Trust kupitia Bank M.

Aliongeza kuwa TRA haikuzingatia ukweli kwamba Joha Trust na yeye ni vitu viwili tofauti, huku akisisitiza kwamba fedha hizo zilikuwa ni kwa ajili ya Joha.

Hata hivyo, wakili wa TRA, Noah Tito ilipinga madai ya Profesa Tibaijuka akidai kuwa utetezi wake hauna msingi kwani fedha hizo ziliingia kwenye akaunti binafsi ya Profesa Tibaijuka na siyo ya Joha Trust.

No comments: