Seleiman Jafo Amemvua Madaraka Meneja wa Mamlaka ya Maji Mji Mdogo wa Kisarawe - LEKULE

Breaking

2 Mar 2016

Seleiman Jafo Amemvua Madaraka Meneja wa Mamlaka ya Maji Mji Mdogo wa Kisarawe


Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleiman Jafo amemvua madaraka Meneja wa Mamlaka ya Maji Mji Mdogo wa Kisarawe mkoani Pwani, Listen Materu kwa kile alichodai ameshindwa kusimamia majukumu yake kikamilifu.

Pia, Jafo ameuagiza uongozi wa halmashauri hiyo kuondoa kero zinazolalamikiwa na wananchi hasa idara za ardhi, afya na elimu.

Akisikiliza kero za wapigakura wake juzi, Jafo alisema uchunguzi alioufanya ameubaini kwa miaka mitano iliyopita kuwa baadhi ya watendaji wa vitengo na idara wa halmashauri hiyo walikuwa hawawajibiki kwa makusudi, lengo lao lilikiwa ni kujenga chuki baina ya mbunge na wananchi jambo ambalo limefikia kikomo.

“Kuna watu waligeuza wilaya hii kama shamba la bibi, walikuwa wanatumia mali za umma kwa kufanya ubadhirifu sasa wasiseme kuwa wamesalimika, kama wamehama au wamehamishwa tutawafuata kokote walipo na watawajibishwa kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Naibu waziri huyo alisema, kuwavua madaraka na kuwawajibisha watendaji wabovu hakutaishia kwa watumishi waliopo wilayani hapa, bali hata waliofanya ubadhirifu na kuhama au kuhamishiwa maeneo mengine.


Katika kuboresha wilaya hiyo na kuharakisha maendeleo, Jafo alisema ni wajibu wa halmashauri kuhakikisha inatenga maeneo ya ujenzi wa stendi, machinjio na utekelezaji wake ufanyike haraka na kuwataka iwapo watakabiliwa na changamoto za kukwamishwa mpango huo wasisite kuwasiliana naye.

No comments: